Sunday, July 29, 2012

WABUNGE MAFISADI WATAJWA.....

SPIKA AVUNJA KAMATI YA NISHATI, WAZIRI AELEZA WALIVYOITAFUNA TANESCO.....
WAKATI wabunge wakitoa tuhuma nzito dhidi ya wenzao wanaodaiwa kujihusisha na ufisadi ndani ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), imebainishwa kuwa wabunge wenye tabia hiyo ni watano, watatu kutoka chama tawala CCM na wawili upinzani.

Habari zilizopatikana jana mjini Dodoma zimeeleza kuwa baadhi ya wabunge hao wanatoka katika Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini, huku wengine wakitoka Kamati ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma.

Kwa mujibu wa taarifa hizo, wabunge hao wamedaiwa kuwa wamekuwa wakitumia nafasi zao za ubunge na ujumbe wa kamati kufanya biashara na Tanesco na kutetea mafisadi ndani ya shirika hilo la umma.

Gazeti hili limefanikiwa kupata majina ya wabunge hao, ambayo leo hatutayataja kwa sababu za kitaaluma.

Baadhi ya wabunge waliochangia hoja hiyo bungeni juzi na jana walisema kuwa, wanawafahamu wabunge hao kwa majina, lakini hawapendi kuwataja kwa kuwa siyo wakati mwafaka.

Moto wa kutaka kutajwa kwa majina ya wabunge hao ulikolezwa jana na Mbunge Vita Kawawa wa Namtumbo(CCM) aliyeomba Mwongozo wa Spika, akitaka jambo hili lijadiliwe na Bunge na kupendekeza kuwa, Kamati za Bunge zinazotuhumiwa kwa rushwa zivunjwe.

“Waheshimiwa wabunge wamejadili suala hili kwenye wizara, lakini kwa mujibu wa kifungu cha 55 (3)f mbunge au waziri anaweza kutoa hoja ili jambo fulani lijadiliwe. Sasa naomba kutoa hoja ya kujadili suala hilo," Kawawa alisema.

Aliliomba pia Bunge likubali kuivunja na kuiunda upya Kamati ya Nishati na Madini na kamati nyingine zilizolalamikiwa kwa rushwa. Hoja hiyo iliungwa mkono na wabunge.

Baada ya hoja hiyo kuungwa mkono Spika wa Bunge, Anne Makinda alisimama na kukubali hoja hiyo ya Kawawa na kutangaza kuivunja Kamati ya Nishati na Madini.

Spika Makinda alisema ameiagiza Kamati ya Haki, Kinga na Maadili ya Bunge kutengeneza kanuni za kuwadhibiti wabunge wenye tabia hiyo ya kupokea rushwa kutoka kwa watu mbalimbali ili kutimiza matakwa yao binafsi.

"Ninakubali kuivunja Kamati ya Nishati na Madini na zingine ambazo zitatajwa kwenye tuhuma hizo. Nalipeleka pia suala hilo kwenye Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge, halafu kama ni kutajwa (wabunge hao), basi tutapata mwongozo wa kamati hiyo." alisema Spika Makinda na kuongeza:

"Nasema kwa dhati kabisa, kitendo hiki hakikubaliki ndani ya Bunge hili. Wabunge mkae vizuri. Kama kuna baadhi yetu wanaenda huku na huku kujitafutia masilahi binafsi, tutawezaje kuisimamia Serikali?"

Mbunge Zedi
Baada ya Spika kutangaza kuvunja Kamati ya Nishati na Madini, Mwenyekiti wa Kamati ya Nishati na Madini, Seleman Zedi alisema kuwa ameshtushwa na uamuzi huo na anasubiri uamuzi wa Kamati ya Haki, Kinga na Maadili ya Bunge.

"Nimeshtushwa sana na uamuzi huo, lakini tusubiri Kamati ya Haki, Kinga na Maadili ya Bunge," alisema Zedi.

Waziri Muhongo
Akihitimisha hoja ya wizara yake bungeni jana, Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo alisema kuwa baadhi ya wabunge ambao wanashiriki kwenye vikao vya uamuzi vya Tanesco kama wajumbe, wamekuwa wakilihujumu shirika hilo kwa njia mbalimbali ikiwamo kufanya nalo biashara.

"Shirika liliwahi kulipa Pauni za Uingereza 50,000 kwa ajili ya kununua vipuri, lakini kilicholetwa nchini ni masanduku ya misumari,” alisema Profesa Muhongo na kuongeza;

“Hata katika nguzo za umeme kuna biashara inaendelea. Tunajua kuwa nguzo hizo zinazalishwa Iringa na kupelekwa Mombasa kisha kurudishwa nchini kwa maelezo kwamba zimetoka Afrika Kusini."

Waziri Muhongo alisema kuwa mbali na ufisadi huo, baadhi ya wabunge ambao ni wajumbe wa Kamati ya Nishati na Madini wamewahi kuliuzia shirika hilo matairi ya magari kwa bei kubwa, bidhaa ambayo hata hivyo alisema haina ubora unaokubalika.

"Baadhi ya wabunge wanafanya biashara na Tanesco; niseme tu kuwa, hii siyo sahihi. Lakini niombe kwamba mjadala huu tuufunge kwa sababu, tayari tumekabidhi suala hilo kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG)" alisema Waziri Muhongo.

Waziri Muhongo pia alizungumzia jinsi baadhi ya watu na kampuni zinavyoiibia Tanesco kupitia mita za Luku ambapo aliwataja watu hao kuwa ni pamoja na Shule za St. Mary's zinazodaiwa Sh10.5 milioni, Access Bank, Tawi la Tabata Matumbi Sh13.8 milioni na Hoteli ya Akudo Paradaise ya Kariakoo inayodaiwa Sh25.5 milioni.

Alisema kuwa baada ya kubainika kwa wadaiwa hao hutumia umeme kinyume na utaratibu,wahusika wote walikamatwa na kufikishwa kituo cha polisi baada ya kufanyika kwa uchunguzi.

“Baada ya kufanya uchunguzi na kubaini kuwapo kwa watu wanaotumia umeme bila kulipia na kuisababishia Tanesco hasara, tumeamua kuwachukulia hatua ikiwamo kuwafikisha polisi,” alisema Profesa Muhongo na kuongeza:

“Inaonyesha wazi kwamba wizi wa umeme wa Luku umekuwa ukifanyika mara kwa mara na kwamba baada ya kuwakamata hawa, uchunguzi utaendelea na wengine watakaobainika watachukuliwa hatua za kisheria.”

Jenista Mhagama

Katibu wa Wabunge wa CCM, Jenista Mhagama alisema kuwa, amepokea kwa masikitiko taarifa hizo za wabunge wa CCM kuingia katika tuhuma hizo, lakini akasema namna nzuri ya kushughulikia tatizo hilo ni vyombo vya dola kufanya uchunguzi makini ili kujiridhisha na kisha hatua za kisheria kufuatwa.

"Ni taarifa mbaya kwa kweli, lakini mimi niiombe Serikali itusaidie kufanya uchunguzi ili ukweli ubainike na hatua zichukuliwe," alisema Mhagama.

Mbunge Silinde
Naye Katibu wa Wabunge wa Chadema, David Silinde alisema: "Kwa kuwa tumesikia, kama kambi tutafanya uchunguzi juu ya tuhuma hizo. Tutakaa kikao cha kuamua nini cha kufanya. Pia tutatoa tamko juu ya mwenendo mzima wa hizi tuhuma na Bunge kwa ujumla.”

Zitto
Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Mashirika ya Umma ambayo imeunganishwa kwenye tuhuma hizo, Zitto Kabwe, alisema tuhuma hizo anazisikia, lakini anaziona kama siasa za majitaka kwa sababu zinarushwa bila ushahidi wowote.

"Hakuna hata mbunge mmoja aliyesimama kusema nani amehongwa nini. Mimi binafsi sijahongwa na mtu yeyote wala mimi sijamtetea mtu isipokuwa natetea taratibu kufuatwa," alisema.

Zitto alibainisha kuwa anaamini tuhuma hizo zimetokana na hasira za yeye kupinga posho za wabunge na sasa wameona hilo ndilo eneo la kumkomoa.

"Kwa kuwa ‘my conscious is clear’, (dhamira yangu safi) sina mashaka, uzushi, uongo na siasa za majitaka hizi zitaumbuliwa na ukweli. Hata hivyo, kwa kuwa tuhuma hizo zinasemwa juu juu tu, tutataka vyombo vya dola vichunguze na ikithibitika hatua zichukuliwe," alisema na kuongeza:

"Kwangu mimi naona hizi ni siasa za urais na hasira za posho. Wenye kutaka urais wa vyama vyote na wapambe wao, wameungana kunichafulia heshima yangu. Wabunge wenye njaa ya posho, wameungana kunikomoa. Ukweli una tabia ya kutopenda kupuuzwa. Mwalimu Nyerere (Julius) alisema katika andiko lake la 'Tujisahihishe'.”

Mbunge huyo wa Kigoma Kaskazini(Chadema) alishauri pia Spika wa Bunge kutumia Kamati ya Maadili kuchunguza tuhuma hizo kwa kuwa hazipaswi kuachwa zikapita hivihivi.

John Cheyo
Mwenyekiti wa Kamati ya Hesabu za Serikali, John Cheyo alisema anasikitika kuona Bunge ambalo kimsingi ni kitovu cha uadilifu limeanza kuvamiwa na mafisadi.

"Very unfortunate, (bahati mbaya sana) Bunge ambalo ni kilele cha uadilifu, nyumba ya waheshimiwa, ambako kunatarajiwa high level of intergrity (uadilifu wa hali ya juu), kuanza kutumika kama perpets (vibaraka) wa mafisadi," alisema.

Cheyo aliongeza: "Ninalaani sana kitendo hicho, lakini niwaambie viongozi wapya wa Wizara ya Nishati na Madini kuwa, waendelee kufanya kazi kwa uadilifu na nguvu yao ni wabunge wengi wema, ambao watawaunga mkono. Wasikate tama," alisema.

Mjadala ya wabunge

Mbunge wa Maswa Magharibi (Chadema), John Shibuda aliliomba Bunge kufanya uchunguzi ili kuwabaini wabunge wanaojihusisha na vitendo vya rushwa.

Alisema baadhi ya wabunge wanatumia nafasi zao vibaya kwa kujihusisha na vitendo vya rushwa ili kuiyumbisha Serikali.

“Namwomba Spika na timu yake yote ikaona kuna haja ya kufanya uchunguzi kwa wabunge ili kuweza kuwabaini wanaotumia nafasi zao vibaya kwa kujihusisha na vitendo vya rushwa ilikuiyumbisha Serikali ,” alisema Shibuda

Mbuge Kangi

Naye Mbunge wa Mwibara, Kangi Lugora alitaka Waziri wa Nishati na Madini awataje wabunge aliowatuhumu ili kuonyesha usawa hasa baada ya kuwataja kwa majina watuhumiwa wengine katika ufisadi wa Tanesco na wale wanaoliibia umeme shirika hilo la umma.

"Tunaomba waziri asema kwa nini asiwataje hao wengine wakati tayari ametutajia kina Freddy na Veronica William Mhando na taasisi za St Mary? " alihoji.

Hoja hiyo ya Lugora ilitupwa na Spika wa Bunge Anne Makinda aliyesema kuwa jambo hilo lina taratibu zake.

Kamata
Vicky Kimata (Viti Maalumu) nusura amwage machozi bungeni juzi jioni, alipozungumza kwa uchungu kupinga hatua ya wabunge hao kujihusisha na ufisadi, huku akieleza kuwa nchi imefika pabaya.

'Watanzania tumefikia hapo! Watu wanatengeneza mgawo wa umeme ili kujipatia hela, Jamani...jamani.. Hammwogopi hata Mungu!"

Said Mussa Zuberi alipendekeza itungwe sheria ya kuwanyonga mafisadi na wahujumu uchumi kwa kuwa matendo hayo pia ni uuaji.

"Katika taifa letu tuna wadudu sijui tuwaite mchwa ambao wanaharibu yaliyotengenezwa kwa maslahi yao. Nawashauri wananchi kwa kuwa sasa tuko kwenye suala la Katiba, wasisahau kupitisha sheria ili watu wahujumu uchumi tuwaue, tena kwa risasi.

Monday, July 23, 2012

Dar Talk" Video ya Utupu ya Agness Masogange yavuja Mtandaoni......

BAADA ya kuandamwa na skendo kibao za kutoka na vigogo kisura wa video za wasanii wa bongo,Agnes Gerald maarufu kama Agnes Masogange, ameonekana kwenye mkanda wa picha ya ngono ambao umesambaa mtaani huku ikiwa dili kwa watu wanaotaka kuona umbo la mwanadada huyo.

Mkanda huo unaomuonesha mwanadada huyo akiwa mtupu, huku utata mkubwa ukizunguka kujua ni kitu gani kilichosababisha hadi kusambazwa kwa video hiyo.

Agnes katika pozi

Mtandao wa DarTalk, ulifanikiwa kupata video hiyo ambayo mwanadada huyo ameonekana na kijana mmoja ambaye bado hajafahamika jina lake. Baadhi ya videos za bongo flava ambazo amewahi kuong’aa ni pamoja na ‘Magube gube’ ya Barnaba , Masogange ya Belle9 na nyingine nyingi.

Baada ya kupatatikana kwa video hiyo mtandao huu ulijaribu kumsaka Agnes ili kufafanua uwepo wake ndani ya video hiyo lakini hakuweza kupatikana kwenye simu yake ya mkononi.

Watanzania 100 wafungwa China.....................

UKAHABA na usafirishaji wa dawa za kulevya unaofanywa na baadhi ya Watanzania ni moja ya dosari zinazotia doa uhusiano kati ya Tanzania na China.

Watanzania zaidi ya 100 wako kwenye magereza ya China wakitumikia vifungo kwa makosa ya kukutwa na dawa za kulevya, huku wasichana wanane wakirejeshwa nyumbani siku chache zilizopita kutokana na ukahaba.

Balozi wa Tanzania nchini China, Philip Marmo alibainisha hayo mwishoni mwa wiki iliyopita katika mkutano uliofanyika nyumbani kwake jijini hapa.

Mkutano huo uliambatana na chakula cha mchana, ukiwa ni maalumu kwa ajili ya Watanzania waliokuwa wakihudhuria Mkutano wa Tano wa Mawaziri wa Ushirikiano kati ya China na Tanzania (FOCAC) uliofanyika Alhamisi na Ijumaa wiki iliyopita.

Mkutano huo ulihudhuriwa pia na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Gregory Teu, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, John Haule na wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Balozi Herbert Mhango.

Aidha, walikuwapo watendaji wakuu kadhaa wa mashirika ya umma, taasisi za umma, sekta binafsi na wafanyabiashara wa Tanzania. Balozi Marmo alisema Tanzania inajivunia uhusiano wa muda mrefu na China tangu miaka ya sitini, ilipofungua ubalozi wake Aprili 26, 1964, lakini katika siku za karibuni umekumbwa na dosari hizo mbili. “Kwa kweli hili la dawa za kulevya, linaumiza vichwa sana.

Hapa ukiwa na dawa za kulevya hufiki popote, wako makini sana. Ukikamatwa hakuna msamaha, adhabu kubwa ni kifo, kwao ni kosa kubwa,” alisema.

Balozi Marmo aliongeza: “Dawa za kulevya kwao ni suala la usalama wa Taifa, ni vigumu kuanzisha mjadala katika suala hili. Katika siku za karibuni, kumekuwa na ongezeko la vijana wetu wanaoshughulika na mihadarati.”

Alisema cha kushangaza vijana hao wanapokamatwa, pasipoti zao huonesha kuwa hawatoki Dar es Salaam, bali katika miji mingine duniani.

“Halafu si kwamba hawa wanaokamatwa wanatoka Dar es Salaam, hapana … utakuta wanatoka Istanbul, Ankara, Rio de Janeiro, Pakistani; baadaye, ndio unajua wanasema tunatoka Kinondoni, Magomeni Mapipa, Tanga, Zanzibar na Kigoma,” aliongeza Balozi.

“Hivi sasa wako Watanzania zaidi ya 100 katika jela za China. Masikini wanatumiwa tu, wengine na wafanyabiashara wakubwa tu, wengine watoto wa wakubwa,” alibainisha zaidi Balozi Marmo. Alisema dosari nyingine katika siku za karibuni, ni wasichana kutoka Tanzania kujihusisha na biashara ya ukahaba China.

“Kuna hili la wanawake wetu kujihusisha na ukahaba … hapa haikubaliki, tayari wapo wanane wanarudishwa nyumbani, wamepewa siku nane za hifadhi kabla ya kuondoka,” alisema Balozi Marmo. “Wenyeji wanatuheshimu, wenzao wa Kenya na Uganda wamepewa siku tatu tu. Kwa kweli, hali hii inaharibu uhusiano wetu mzuri na China.”

Alisema Wachina wanaipenda sana Tanzania na wanaiona Tanzania kuwa sehemu nzuri ya kuwekeza na kufanya biashara, hivyo ni vyema fursa hiyo ikatumiwa vizuri badala ya kuchafua jina la nchi.

Alikerwa pia na alichoeleza kuwa ni biashara ndogo zinazofanywa na Watanzania, hasa wanawake kwa kubeba mabegi, badala ya kuchangamkia biashara kubwa na wenzao wa Taifa hili la Asia.

“Biashara tunazofanya ni ndogo sana, akinamama wanabeba mabegi tu, hii si biashara. Tulipaswa kufanya biashara ya makontena kupeleka nyumbani,” alieleza Balozi Marmo ambaye yuko Beijing takriban miezi mitatu sasa tangu ateuliwe kushika wadhifa huo.

Balozi Marmo aliwataka Watanzania kutumia urafiki na uhusiano mzuri kati ya Tanzania na China kufanya biashara kwa manufaa yao na Taifa. Mwito huo uliungwa mkono na mawaziri Membe na Teu ambao waliwataka wafanyabiashara hao na Watanzania kwa jumla, kuchangamkia fursa zinazopatikana China.

Katika miaka ya karibuni, China imekuwa mshirika mpya wa mataifa ya Afrika katika maendeleo, na imekuwa ikifadhili miradi mingi kuanzia elimu hadi masuala ya michezo na utamaduni.

Monday, July 2, 2012

Gari La Jackline Wolper Lakamatwa...........

LILE gari la kifahari aina ya BMW X6 lenye namba za usajili T 574 BXF linalomilikiwa na staa wa sinema za Bongo, Jacqueline Wolper Masawe limedakwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
Kwa mujibu wa ofisa mmoja wa TRA ambaye hakutaka jina lake lichorwe gazetini, gari hilo la kisasa lilikamatwa Juni 28, 2012 kupitia Kampuni ya Mnada ya Majembe kutokana na sababu kadha wa kadha.

SABABU ZAANIKWA
Akiendelea kufunguka, afisa huyo alisema kuwa sababu ya kwanza ni kuhisiwa kuwa gari hilo liliingizwa nchini kinyemela kutokana na vielelezo vyake vya kwenye kadi kupitia kwenye vyombo vya habari, ndipo taa nyekundu ikawaka ndani ya vichwa vya maafisa wa TRA na kuanza kulifuatilia.
Alidai kuwa mbali ya kuingia nchini kinyemela, lakini BMW hilo halijalipiwa ushuru zaidi ya miaka mitano iliyopita kwa mujibu wa vielelezo vyake.

MPANGO WA KULIKAMATA ULIVYOSUKWA
Kwa mujibu wa ofisa huyo, ili kufanikisha zoezi la kulikamata gari hilo, vijana kutoka kampuni ya Majembe waliingia mzigoni kulisaka ambapo kuna mtu alipiga kambi jirani na makazi ya Wolper, Mbezi Beach jijini Dar.
Ilisemekana kuwa vijana hao walikuwa na kazi moja tu, kuhakikisha anapotoka Jack wanamfuatilia hatua kwa hatua hadi mahali atakapokwenda kupiga kambi na kulitia mikononi.
“Haikuwa kazi rahisi maana muda mrefu alikuwa haonekani nalo, ndipo mpango huo ulipokuja kukamilishwa kwa njia ya kumfuatilia anapotoka kwake hadi mahali lilipokamatwa maeneo ya katikati ya Jiji la Dar,” alisema.

Akaendelea kudai: “Unajua hawa mastaa wetu kuna vitu wanavifanya bila kujua madhara yake, kitendo cha Wolper kuonesha kadi ya gari kwa waandishi wa habari huku anafahamu ina mapungufu kibao ndiyo sababu kuu ya gari hilo kuanza kufuatiliwa.”

MH! ETI USHURU MILIONI 70?
Taarifa nyingine ya kushtua ni kwamba ilidaiwa kuwa kuwa TRA peke yake inadai Sh. milioni 70 za ushuru.
“Si fedha ndogo zinazodaiwa na TRA, kwa hesabu ya harakaharaka ni zaidi ya Sh. milioni 70 ambazo zinatakiwa kulipwa.”
Baada ya The Biggest IQ Paper, Ijumaa Wikienda kujiridhisha kuwa gari hilo limedakwa, lilimuendea hewani Wolper lakini hakuweza kupokea simu hadi gazeti linakwenda mitamboni.

Picha za Harusi Ya Msanii wa Bongo Flava Black Rinho....

BIG UP RHINO....MTOTO MZURI!!!!

Wanafunzi wasema kuuza Rambo kunalipa sio shule.........

BAADHI ya watoto wanaostahili kwenda shuleni kuhudhuria masomo, wamekuwa ni kero kwenye masoko mbalimbali jijini Arusha kutokana na kuuza mifuko ya plastiki maarufu Rambo.

Aidha, watoto hao wamedai uuzaji wa rambo hizo kunalipa zaidi badala ya kuhudhuria masomo yasiyo na manufaa kwao na wengine wanalinda magari ya wananchi wanaofika sokoni kununua mahitaji yao.

Mwandishi wa habari hii alitemb
elea soko la Kilombero na Soko Kuu na kukuta watoto hao wanaostahili kwenda shule nyakati za asubuhi wakikimbilia wateja na kuwauzia mifuko ya Rambo kwa Sh 100 kisha kung’ang’ania kubea mizigo isiyoendana na uzito/umri waliokuwa nao.

Mmoja kati ya watoto hao, Emmanuel Joel (11) alisema anasoma darasa la tatu katika shule ambayo hakutaka kuitaja, lakini kutokana na mazoea ya kuuza mifuko hiyo na kupata faida zaidi, ameona shuleni hatapata maendeleo na kuamua kujikita kwenye biashara hiyo ili apate fedha za kujikimu.

Alisema familia yao sio duni, lakini anauza mifuko hiyo kutokana na kupata fedha na asubuhi anavaa nguo za shule na kwenda shule, lakini akifika eneo fulani anajificha kisha anabadili nguo na kwenda sokoni kuuza mifuko hiyo na muda wa kurudi shule ukifika anakwenda nyumbani kama kawaida.

“Mazaa hii kazi inalipa kuliko masomo hivyo nimeona bora niifanye ili nipate fedha nikiuza mifuko yote napata faida ya shilingi elfu mbili au elfu mia tano kwa siku na nikibeba mizigo, bei ni maelewano kati yangu na mwenye mizigo hivyo ndio maisha kwani sioni sababu ya kusoma wakati napata fedha,” alidai.

Hata hivyo, jitihada za Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Jiji la Arusha, Estomih Chang’a za kutoa matangazo yanayowataka watu wazima kutoajiri watoto au kununua Rambo zinazouzwa na watoto hao, zimegonga mwamba kutokana na watoto hao kufanya biashara kama kawaida ingawa matangazo wanayasikia.

Vigogo wa Suma JKT kortini kwa ufisadi........

ASKARI saba wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) wakiwamo Luteni Kanali watatu, wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam wakikabiliwa na mashitaka ya kuhamisha na kupitisha Sh bilioni 3.8 kwa ajili ya ununuzi wa mali chakavu. Washitakiwa hao walifikishwa mahakamani hapo jana asubuhi na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), wakiwa kwenye gari aina ya Toyota Land Cruiser lenye namba za usajili T529 ASM lenye vioo vyeusi wakisindikizwa na gari lenye namba DFP 8763. Walisomewa mashitaka saba na mawakili kutoka Takukuru, Donasian Kessy na Ben Linkolin mbele ya Hakimu Mkazi Aloye Katema. Washitakiwa wenye cheo cha Luteni Kanali ni Mkohi Kichogo, Paul Mayavi na Felix Samillan ambaye ni Mkuu Miradi wa Suma JKT. Wengine ni Kanali Ayoub Mwakang’ata, Sajini John Laizer, Meja Peter Lushika na Meja Yohana Nyuchi. Wakili Kessy alidai kuwa, Machi 5, 2009 katika Ukumbi wa Mikutano wa Shirika la Suma JKT, washitakiwa wakiwa wajumbe wa Bodi ya Suma JKT, walijifanya wajumbe wa Bodi ya Kampuni ya Takopa inayoundwa kwa ubia kati ya Serikali ya Korea Kusini na Suma JKT. Alidai lengo la kujifanya wajumbe wa Bodi ya Takopa, lilikuwa kupitisha fedha kutoka kampuni hiyo kwenda Suma JKT kwa ajili ya ununuzi wa magari na mitambo ya ujenzi chakavu bila idhini ya Bodi ya Wakurugenzi wa kampuni hiyo. Wakili Kessy alidai kuwa washitakiwa walitumia vibaya ofisi kupitisha fedha hizo kwa ajili ya ununuzi wa magari pamoja na mitambo hiyo bila kufuata kifungu cha 58 (3) cha Sheria ya Manunuzi ya Umma. Aliendelea kudai katika mashitaka ya tatu yanayowakabili Luteni Kanali Samillan na Luteni Kanali Kichogo kuwa, Machi 16, 2009 walihamisha Sh bilioni 2.8 kupitia hundi namba 000010 kutoka akaunti ya Takopa namba 0111030331753 kwenda akaunti ya Suma JKT 01110307094 katika Benki ya Taifa ya Biashara (NBC). Ilidaiwa kuwa Aprili 3, 2009, wakijidai wajumbe wa Bodi hiyo ya Takopa walihamisha Sh milioni 489.7, Aprili 4 walihamisha Sh milioni 269.5, Mei 4, mwaka huo walihamisha Sh milioni 350 kutoka akaunti ya Takopa kwenda akaunti ya Suma JKT bila kuzingatia Kanuni ya 156 ya Sheria ya Fedha za Umma. Katika mashitaka ya saba yanayowakabili washitakiwa wote, ilidai kuwa kati ya Machi na Mei mwaka 2009 jijini Dar es Salaam, washitakiwa walipanga njama za kuhamisha fedha kutoka katika taasisi ya Takopa kwenda kwenye akaunti ya Suma JKT bila kufuata Kanuni 156 ya Sheria ya Fedha za Umma. Washitakiwa wote walikana kutenda makosa hayo na upande wa mashitaka ulidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo umekamilika na kuwa hawana pingamizi la dhamana endapo washitakiwa watakidhi masharti yatakayotolewa na Mahakama. Hakimu Katemana aliwataka washitakiwa kuwa na wadhamini wawili wa kuaminika watakaosaini hati ya Sh milioni 25 kila mmoja. Washitakiwa walitimiza masharti na kuachiwa kwa dhamana hadi Agosti mosi, mwaka huu. Hata hivyo, baada ya washitakiwa hao kufikishwa mahakamani hapo, hawakuwekwa mahabusu kama ilivyo kawaida kwa washitakiwa wengine, walikaa kwenye gari hadi saa 7 mchana waliposomewa mashitaka yao.