UKAHABA na usafirishaji wa dawa za kulevya unaofanywa na baadhi ya Watanzania ni moja ya dosari zinazotia doa uhusiano kati ya Tanzania na China.
Watanzania zaidi ya 100 wako kwenye magereza ya China wakitumikia vifungo kwa makosa ya kukutwa na dawa za kulevya, huku wasichana wanane wakirejeshwa nyumbani siku chache zilizopita kutokana na ukahaba.
Balozi wa Tanzania nchini China, Philip Marmo alibainisha hayo mwishoni mwa wiki iliyopita katika mkutano uliofanyika nyumbani kwake jijini hapa.
Mkutano huo uliambatana na chakula cha mchana, ukiwa ni maalumu kwa ajili ya Watanzania waliokuwa wakihudhuria Mkutano wa Tano wa Mawaziri wa Ushirikiano kati ya China na Tanzania (FOCAC) uliofanyika Alhamisi na Ijumaa wiki iliyopita.
Mkutano huo ulihudhuriwa pia na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Gregory Teu, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, John Haule na wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Balozi Herbert Mhango.
Aidha, walikuwapo watendaji wakuu kadhaa wa mashirika ya umma, taasisi za umma, sekta binafsi na wafanyabiashara wa Tanzania. Balozi Marmo alisema Tanzania inajivunia uhusiano wa muda mrefu na China tangu miaka ya sitini, ilipofungua ubalozi wake Aprili 26, 1964, lakini katika siku za karibuni umekumbwa na dosari hizo mbili. “Kwa kweli hili la dawa za kulevya, linaumiza vichwa sana.
Hapa ukiwa na dawa za kulevya hufiki popote, wako makini sana. Ukikamatwa hakuna msamaha, adhabu kubwa ni kifo, kwao ni kosa kubwa,” alisema.
Balozi Marmo aliongeza: “Dawa za kulevya kwao ni suala la usalama wa Taifa, ni vigumu kuanzisha mjadala katika suala hili. Katika siku za karibuni, kumekuwa na ongezeko la vijana wetu wanaoshughulika na mihadarati.”
Alisema cha kushangaza vijana hao wanapokamatwa, pasipoti zao huonesha kuwa hawatoki Dar es Salaam, bali katika miji mingine duniani.
“Halafu si kwamba hawa wanaokamatwa wanatoka Dar es Salaam, hapana … utakuta wanatoka Istanbul, Ankara, Rio de Janeiro, Pakistani; baadaye, ndio unajua wanasema tunatoka Kinondoni, Magomeni Mapipa, Tanga, Zanzibar na Kigoma,” aliongeza Balozi.
“Hivi sasa wako Watanzania zaidi ya 100 katika jela za China. Masikini wanatumiwa tu, wengine na wafanyabiashara wakubwa tu, wengine watoto wa wakubwa,” alibainisha zaidi Balozi Marmo. Alisema dosari nyingine katika siku za karibuni, ni wasichana kutoka Tanzania kujihusisha na biashara ya ukahaba China.
“Kuna hili la wanawake wetu kujihusisha na ukahaba … hapa haikubaliki, tayari wapo wanane wanarudishwa nyumbani, wamepewa siku nane za hifadhi kabla ya kuondoka,” alisema Balozi Marmo. “Wenyeji wanatuheshimu, wenzao wa Kenya na Uganda wamepewa siku tatu tu. Kwa kweli, hali hii inaharibu uhusiano wetu mzuri na China.”
Alisema Wachina wanaipenda sana Tanzania na wanaiona Tanzania kuwa sehemu nzuri ya kuwekeza na kufanya biashara, hivyo ni vyema fursa hiyo ikatumiwa vizuri badala ya kuchafua jina la nchi.
Alikerwa pia na alichoeleza kuwa ni biashara ndogo zinazofanywa na Watanzania, hasa wanawake kwa kubeba mabegi, badala ya kuchangamkia biashara kubwa na wenzao wa Taifa hili la Asia.
“Biashara tunazofanya ni ndogo sana, akinamama wanabeba mabegi tu, hii si biashara. Tulipaswa kufanya biashara ya makontena kupeleka nyumbani,” alieleza Balozi Marmo ambaye yuko Beijing takriban miezi mitatu sasa tangu ateuliwe kushika wadhifa huo.
Balozi Marmo aliwataka Watanzania kutumia urafiki na uhusiano mzuri kati ya Tanzania na China kufanya biashara kwa manufaa yao na Taifa. Mwito huo uliungwa mkono na mawaziri Membe na Teu ambao waliwataka wafanyabiashara hao na Watanzania kwa jumla, kuchangamkia fursa zinazopatikana China.
Katika miaka ya karibuni, China imekuwa mshirika mpya wa mataifa ya Afrika katika maendeleo, na imekuwa ikifadhili miradi mingi kuanzia elimu hadi masuala ya michezo na utamaduni.
No comments:
Post a Comment