Saturday, August 4, 2012

Spika aunda kamati maalum kuchunguza ufisadi bungeni...

KAMATI YA MAADILI YAWEKWA KANDO,KUKAMILISHA KAZI KWA WIKI MBILI...

SAKATA la tuhuma za ufisadi bungeni limeingia katika hatua mpya, baada ya Spika wa Bunge, Anne Makinda kuamua kuunda Kamati ndogo ya watu watano kuchunguza tuhuma za baadhi ya wabunge kuhongwa, kwa lengo la kushawishi uamuzi unaofaa kuchukulia katika chombo hicho cha kutunga sheria.

Uamuzi huo ambao Spika aliutangaza jana baada ya kipindi cha maswali na majibu Bungeni, unauweka kando ule wa awali, ambao ulikuwa ni kulipeleka suala hilo katika Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge, ambapo alikuwa ameahidi kuwaengua wote watakaoonekana kuwa, wana mgongano wa kimaslahi na suala linalotakiwa kuchunguzwa.

Habari ambazo gazeti hili lilizipata zinadai kuwa, hadi jana wakati Makinda akichukua uamuzi huo, Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge ilikuwa imeishaanza kazi kwa kufanya vikao kadhaa vya kuainisha watu ambao walipaswa kuitwa ili kutoa ushahidi na wengine kwa ajili ya kujibu tuhuma dhidi yao.

Makinda alisema Kamati hiyo itakayoongozwa na Mbunge wa Mlalo, Brigedia Jenerali Hassan Ngwilizi, itachunguza ukweli wa tuhuma hizo na kutoa majibu kwake ndani ya siku 14 kuanzia jana.

Alisema ameamua kufanya mabadiliko ya namna ya kushughulikia tuhuma hizo ili kutenda haki kutokana na unyeti wa suala hilo.

"Kwa kuzingatia misingi ya haki asili, tumeamua kutomweka mjumbe yeyote wa Kamati ya Nishati na Madini katika kamati hiyo," alisema Spika Makinda na kuongeza;

"Wajumbe wa kamati hiyo ni Mheshimiwa John Chiligati (Manyoni Magharibi), Riziki Omar Juma (Viti maalum), Said Amour Arfi (Mpanda Mjini) na Gosbert Blandes (Karagwe)."

Hata hivyo wajumbe wanne kati ya watano wanatoka ndani ya Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge, isipokuwa Chiligati ambaye anaungana na wenzake akitokea katika Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama.

Spika alibainisha kuwa, kamati hiyo imepewa majukumu ya kuchunguza tuhuma hizo na kujiridhisha kuhusu ukweli wake, kisha kumshauri (Spika) hatua za kuchukua.

Hatua hiyo ya Spika imekuja siku chache baada ya baadhi ya vyama vya siasa na wabunge, kuhoji usafi wa Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge hata ikapewa jukumu la kuchunguza tuhuma hizo.

Baadhi ya vyama vilivyoitilia shaka kamati hiyo ni NCCR Mageuzi, ambacho Mwenyekiti wake, James Mbatia alitaka Kamati hiyo pia ivunjwe na kuchunguzwa kwa tuhuma za ufisadi.

Chama kingine ni Chadema, ambapo mwanachama na Mnadhimu Mkuu wa kambi ya upinzani, Tundu Lissu alitaka zivunjwe kamati kadhaa badala ya kamati ya Nishati na Madini pekee.

Pia Mbunge wa Arumeru Mashariki (Chadema), Joshua Nassari aliomba mwongozo wa Spika akitaka Kamati za Bunge za Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC) na ile ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC), zivunjwe kwani tayari zilishatuhumiwa kwa rushwa.

Hadidu rejea
Spika Makinda alisema kuwa, moja ya majukumu ya msingi ya kamati ya kina Ngwilizi ni kukutana na kukubaliana namna ya kuendesha uchunguzi huo kwa haki na weledi.

"Kamati hiyo itatakiwa kupitia kumbukumbu ya taarifa rasmi za Bunge (Hansard) ili kujua michango ya wabunge wakati wa bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini, kuwaita na kuwahoji mashahidi," alisema Spika Makinda.

Spika Makinda alimtaja Tundu Lissu kuwa ni shahidi muhimu katika uchunguzi huo, kutokana na hatua yake ya kuwataja baadhi ya watuhumiwa katika mkutano wake na waandishi wa habari mjini Dodoma.

Aliwataja mashahidi wengine katika uchunguzi huo kuwa ni Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, wabunge wote waliochangia Hotuba ya Wizara ya Nishati na Madini na kutoa tuhuma za rushwa na mbunge yeyote mwenye ushahidi.

"Tundu Lissu ni shahidi kwa sababu aliwahi kuwataja wabunge hao kwenye mkutano wake na waandishi wa habari na waziri ndiye aliyeanzisha tuhuma hizo bungeni," Spika Makinda alisema.

Aliongeza kuwa, kutokana na unyeti wa suala hilo, kamati hiyo inapaswa kuzingatia Katiba, Sheria, Kanuni za Bunge na weledi wa hali ya juu.

"Sasa waliotaka kuwataja wabunge hao humo bungeni sasa waende wakawataje kwenye kamati hiyo, alisema Spika Makinda," alisema.

Hata hivyo, jana mchana wakati wa kuahirishwa kikao cha Bunge cha mchana mbunge wa Muhambwe (NCCR-Mageuzi), Felix Mkosamali alihoji sababu za kamati hiyo kujaa wabunge watatu wa CCM huku chama chake kikiwa hakina hata mjumbe mmoja.

Lakini, hoja hiyo ilifafanua na mwenyekiti Jenister Mhagama aliyekuwa akiendesha Bunge kwani alisema isingekuwa rahisi kamati hiyo kujaza watu wengi.

No comments:

Post a Comment