Monday, October 22, 2012

Pembe za ndovu kutoka Dar zanaswa Hong Kong......

MAOFISA Forodha wa Hong Kong wamekamata kontena mbili za pembe za ndovu zenye thamani Dola za Marekani 3.4 milioni (wastani wa Sh5.4 bilioni), zinazodaiwa kupelekwa huko zikitokea Tanzania na Kenya.

Pembe hizo, vipande 1,209 vyenye uzito wa tani nne, zilikamatwa juzi nchini humo zikiwa kwenye kontena mbili ambazo ziliwekwa alama kuwa zimebeba plastiki chakavu na maharagwe aina ya roscoco.

Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki akizungumza na gazeti dada la Mwananchi (The Citizen), alisema amepata taarifa za kukamatwa kwa pembe hizo na atatoa maelezo baadaye.

“Nimepata taarifa, lakini siwezi kuzungumzia hilo sasa hivi kwa kuwa tuko katika mchakato wa kuuza akiba ya pembe za ndovu tulizonazo.”

Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori, Paul Sarakikya alisema hana taarifa kuhusu kukamatwa kwa pembe hizo na kuahidi kufuatilia.

“Hatujapata hizo taarifa, kwani wewe umezipata wapi? Gazeti gani hapa Tanzania limeandika habari hizo! Kama hazijaandikwa, ndiyo kwanza wewe unanipa taarifa, hivyo tutafuatilia,” alisema na kuongeza kuwa watawasiliana na Idara ya Polisi wa Kimataifa (Interpol), ili waweze kujua undani wa suala hilo.

Taarifa kutoka Hong Kong zinasema hiyo ni mara ya kwanza kwa kiasi kikubwa kama hicho cha pembe za ndovu kukamatwa nchini humo zikiwa zimefichwa ndani ya mabegi yaliyokuwa na plastiki chakavu pamoja na maharagwe.
Kugundulika kwa pembe hizo imeelezwa kulitokana na taarifa zilizotolewa na maofisa wa Serikali ya China kwa maofisa forodha wa Hong Kong.

Kutokana na tukio hilo, Serikali ya China imewakamata watu saba akiwamo mkazi mmoja wa Hong Kong kuhusiana na pembe hizo.

Kukamatwa kwa pembe hizo kumekuja wakati Serikali ikiwa imeomba upya kwa Umoja wa Mataifa, kuuza akiba yake ya pembe za ndovu zilizotaifishwa ili kupata fedha za kuimarisha ulinzi, kwa lengo la kumaliza tatizo la ujangili.
Ripoti zinaeleza kuwa idadi ya tembo katika Bara la Afrika imepungua kutoka mamilioni katikati ya karne ya 20 hadi kufikia 600,000 mwishoni mwa miaka ya 1980.

Biashara haramu ya pembe za ndovu imetokana na mahitaji makubwa kutoka Bara la Asia na nchi za Mashariki ya Kati, ikidaiwa kuwa hutumika kutengeneza dawa za asili. Bara la Afrika linakadiriwa kuwa na tembo 472,000.

No comments:

Post a Comment