Saturday, August 4, 2012

Wanasayansi waazimia kuuangamiza Ukimwi,,,,,,,,,,,,,,

MBINU MPYA ZA KITAALAMU SASA KUTUMIKA DUNIA NZIMA  ......................

MKUTANO wa Ukimwi uliokuwa unafanyika Washington DC, Marekani umemalizika kwa wajumbe zaidi ya 2,000 kuridhia maendeleo ya kisayansi yaliyofikiwa kwa sasa wakisema ni madhubuti hivyo kutoa azimio la kuungana kuangamiza janga la maradhi hayo duniani. Moja ya maazimio yao ni kuifikisha dunia mahali ambako hakutakuwa na mtu atakayekufa wala atakayekuwa anaishi na Virusi Vya Ukimwi (VVU). Hii inatokana na matumaini ya kisayansi waliyohakikishiwa na watafiti juu ya kuwepo kwa dawa zinazoweza kuzuia maambukizo mapya na ambazo zikitumika kikamilifu zaweza kufanya kazi kama tiba.

Pamoja na kuwepo kwa dawa hizo, wamekiri kuwa mkakati huo hauwezi kufikiwa iwapo dunia haitajenga mshikamano wa pamoja wa kisera, uelimishaji na fedha za kutosha kufanikisha mbinu hizo mpya za kisayansi. Wanasayansi wametahadharisha kuwa kuwepo kwa dawa hiyo siyo tija ya kuumaliza Ukimwi kama mikakati imara haitawekwa dunia nzima. Rais wa Taasisi ya Kijamii ya Kimataifa ya Mapambano dhidi ya VVU (IAS), Dk Elly Katabira alisema yapo mambo mengi ambayo yalithibitishwa kisayansi huko nyuma lakini kwa kuwa hakukuwa na mikakati madhubuti, tatizo hilo limeendelea kuwa janga la dunia.

Dk Katabira ambaye pia ni mmoja wa watafiti wa kisayansi katika Chuo Kikuu cha Tiba cha Makerere, Uganda alitoa mfano wa watoto kuendelea kuambukizwa Ukimwi wanapozaliwa wakati tayari dawa ya kuondoa tatizo hilo ipo. “Ni jambo la kusikitisha kwamba dawa ya kuzuia maambukizo ya VVU tumekuwa nayo tangu miaka 1990 lakini mwaka huu, 2012 takwimu zinaonyesha kuwa watoto zaidi ya 300,000 wataambukizwa VVU wakati wa kuzaliwa,” alisema Dk Katabira, ambaye pia alikuwa ni Mwenyekiti wa mkutano huo wa Ukimwi uliomalizika wiki iliyopita.

Kwa sababu hiyo, akasema silaha za kupambana na Ukimwi kwa sasa zipo lakini kama hakuna mikakati madhubuti ya kuzitumia, bado utaendelea kuwa janga la dunia. Mkutano huo wa kimataifa wa Ukimwi umekuwa ukifanyika kila mwaka ukiwakutanisha wanasayansi na watunga sera kama vile wanasiasa na wadau wa mapambano dhidi ya ugonjwa huo uliogundulika kwa mara ya kwanza mwaka 1981.

Mkutano wa safari hii umeelezewa kuwa ni wa kipekee zaidi ukilinganishwa na ile iliyowahi kufanyika miaka 30 iliyopita kwani kwa mara ya kwanza, umethubutu kutamka wazi, “dawa ya kuangamiza kabisa janga la Ukimwi ipo.” Kutokana na kujiamini huko, mkutano huo umetoka na Azimio linaloitwa la Washington DC ambalo ni la kugeuza kauli ya kuwa “Ukimwi hauna dawa” na kuwa “Ni wakati wa kuangamiza janga la Ukimwi.”

Azimio hilo ambalo tayari limetafsiriwa katika lugha mbalimbali duniani, kikiwemo Kiswahili, linasema: “Kugeuza mkono kwa pamoja: Ilani ya kuangamiza janga la Ukimwi.” Linaeleza: “Tuko katika wakati wa kipekee katika historia ya janga la Ukimwi. Miongo mitatu ya upiganiaji, utafiti na utoaji wa huduma stahimilivu kwa jamii imeifikisha dunia katika hali ambayo haikuwazika miaka iliyopita.” “Kwa sasa kuna uwezekano wa kuanza kuangamiza janga la Ukimwi wakati wetu.

Hasara imekuwa ya kutohesabika… Lakini sasa, kupitia maendeleo mapya ya kisayansi… Tumegundua kwamba inawezekana kukusanya mbinu zilizothibitishwa, ambazo, kama zitatekelezwa ipasavyo, zinaweza kugeuza mkondo wa Ukimwi.” Ingawa tafiti za kisayansi zinaendelea na baadhi zikiwa na matumaini mazuri ya kupata dawa ya chanjo na kuponya waathirika dhidi ya VVU, bado hazijathibitishwa na azimio la mkutano huo limeridhia mbinu zilizowasilishwa na wanasayansi za kuzuia maambukizo.

Imeelezwa kwamba mbinu hizo mpya za kuzuia kusambaa kwa VVU zikitumika kikamilifu siyo tu zitazuia maambukizo mapya, bali zitatibu wale waliokwishaambukizwa. Moja ya mikakati ya kufanikisha azimio hilo ni kuhakikisha duniani kote vinapatikana vifaa bora vya kuchunguza VVU na upatikanaji wa dawa. “Lazima tuongeze rasilimali na bidii yetu kwa kutumia vifaa tulivyonavyo leo kuzuia maambukizo mapya na kuboresha afya ya mamilioni ya watu walio na VVU/Ukimwi. Mamilioni ya maisha yataokolewa,” inaeleza sehemu ya Azimio hilo la Washington DC na kuongeza:

“Lengo la kwanza ni kuangamiza janga la Ukimwi... Liko katika uwezo wetu... Hakuna mtu anapaswa kutengwa ikiwa tunapanga kufikia lengo letu.” Miongoni mwa mambo ambayo azimio hilo linasisitiza kuwa hayana budi kuzingatiwa ili kuleta usawa ni pamoja na kuondoa unyanyapaa, ubaguzi, vikwazo vya kisheria na unyanyasaji wa haki za waathirika na wale walio hatarini. “Unyanyapaa na ubaguzi unazuia juhudi zetu zote na kuzuia utoaji wa huduma muhimu. Tuongeze kwa dhahiri upimwaji wa VVU, utoaji ushauri na uhusiano wa kinga, huduma za kuponya na usaidizi. Kila mtu ana haki ya kujua hali yake ya VVU na kupata matibabu, dawa na usaidizi,” linasisitiza azimio hilo.

Malengo mengine ni kutoa matibabu kwa wanawake wote wajawazito na wanaonyonyesha wanaoishi na VVU na kuangamiza uambukizaji wakati wa kujifungua. Azimio linahamasisha ujengaji wa mtandao mpana wa vita hiyo kwa kusema: “Tuongeze ufikio wa matibabu ya kupunguza makali ya VVU/Ukimwi kwa wote wanaohitaji.

Hatuwezi kuangamiza Ukimwi mpaka mikakati hii iweze kutekelezeka ulimwenguni kote.” Linaongeza: “ Tuharakishe utafiti kuhusu vifaa vipya vya kukinga na kutibu VVU, ikiwa ni pamoja na njia mpya kama vile tiba ya kuzuia maradhi kabla ya kuambukizwa (PrEP) na vizuizi vya vijiumbe maradhi na utoaji bora wa kile tunachojua kinafanya kazi ipasavyo; kuanzia kondomu mpaka matibabu kama kinga.

Tuongeze utafiti wa dawa ya chanjo na dawa ya kuponya. Utafiti ni muhimu kwa kutusaidia kupigana na janga hili.” Tayari Dawa ya Kupunguza Makali ya VVU (ARV) ya Truvada iliyonza kutumika duniani tangu 2004, wiki chache zilizopita ilithibitishwa na Mamlaka ya Chakula na Dawa Marekani (FDA), kuwa ina uwezo wa kuzuia mtu aliyeathirika kumwambukiza mwenzi wake atakayeshiriki naye tendo la ndoa bila kutumia kondomu. Zipo aina kadhaa ya dawa za chanjo na tiba zilizowasilishwa kwenye mkutano huo pamoja na ushahidi wa jinsi zinavyoponya lakini bado hazijathibitishwa kutumika kimataifa.

No comments:

Post a Comment