Saturday, August 4, 2012

Zitto atoa ya moyoni kuhusu madai ya rushwa........

WAKATI shinikizo la kuvunjwa kwa Kamati ya Bunge ya Mashirika ya Umma (POAC), kwa tuhuma za ufisadi likiendelea, Mwenyekiti wake, Zitto Kabwe ameibuka na kukituhumu chama tawala CCM, Serikali na baadhi ya wapinzani akidai kuwa wana uchu wa kuiongoza kamati hiyo na wanaratibu mkakati wa kumchafua.

Kwa sababu hiyo, amepinga maoni ya baadhi ya wabunge wanaotaka ivunjwe na badala yake akasema kama kuna ushahidi wa kutosha dhidi ya vitendo vya rushwa, basi awajibike yeye.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Zitto alisema licha ya mkakati huo, katu hatarudi nyuma katika kutetea masilahi ya taifa kwa kuwa anaamini siku zote uongo hujitenga na ukweli.
“Mchango wa POAC katika Bunge na ustawi wa mashirika ya umma ni bayana na haujawahi kutiliwa shaka. Kamati yetu imeokoa upotevu mkubwa wa mali na fedha za umma kutokana na umakini wake,” alisema Zitto na kuongeza:

“Tumefanya hivyo CHC, Kiwira na kwenye mashirika mengi. Kote huku uadilifu wa kamati hii haujawahi kuhojiwa. Zipo hoja pandikizi za kutaka POAC ivunjwe na haswa zikinilenga mimi binafsi. Nafahamu kiu ya wasioitakia mema nchi yetu kuiona POAC ikivunjwa au sura zikibadilishwa kwa kuwa kamati hii imekuwa mwiba kwa mikakati yao ya kifisadi.”

“Kwa maoni yangu, POAC isihusishwe na tuhuma hizi kwa vyovyote vile. Niko tayari nihukumiwe mimi (Zitto) na siyo kuhusisha wajumbe wengine ambao hawatajwi mahala popote katika tuhuma hizi mbaya sana katika historia ya Bunge letu.”

“Nitakuwa tayari kunusuru Kamati ya POAC na masilahi ya taifa letu kwa kujiuzulu uenyekiti, iwapo itathibitika pasipo shaka kuwa nimehongwa. Kamati ya POAC ni muhimu kuliko mimi.”

Awali, Zitto alisema amelazimika kuzungumzia suala hilo kuufahamisha umma kwamba tuhuma hizo zenye shinikizo la kisiasa zinaelekezwa kwake binafsi na si kamati kwa jumla wake.
“Taarifa hizo, kama kawaida ya uzushi mwingine wowote, zimesambazwa kimkakati na kwa kasi kubwa, kiasi cha kuukanganya umma,” alisema.

Alisema mkakati wa kumuunganisha na baadhi ya wabunge wanaotuhumiwa kupokea rushwa, unatekelezwa kwa njia mbalimbali, ikiwamo kauli za watendaji wa Serikali aliodai wamekuwa wakizieneza kutoa taswira kwamba baadhi hoja zake zinatokana na ushawishi wa rushwa.

Akifafanua tuhuma za ushiriki wake wa rushwa katika sekta ya Nishati na Madini, Zitto alisema baada ya Bodi ya Wakurugenzi ya Tanesco kumsimamisha Mkurugenzi Mkuu, William Mhando, POAC ilimwomba Spika aridhie kamati yake iwaite wajumbe wa bodi hiyo ya Tanesco, CAG na PPRA, kujiridhisha na tuhuma hizo.

“POAC ilimwomba Spika kuwaita wahusika kwa kuwa zilikuwapo tetesi kuwa kusimamishwa kazi kwa mkurugenzi huyo kabla ya Bajeti ya Nishati na Madini kulikuwa na lengo la kufunika ‘madudu’ makubwa zaidi, kwa kulichagiza Bunge na tukio hilo dogo, mkakati ambao naona umefanikiwa sana,” alisema na kuongeza:

“Isitoshe, kamati kujiridhisha na hatua za bodi ni sehemu ya msingi ya utekelezaji wa majukumu yake yaliyowekwa kwa mujibu wa Kanuni za Kudumu za Bunge pia Tanesco ni moja ya mashirika ambayo yanawajibika kwetu kwa hesabu zake na ufanisi wake kwa jumla. Tumefanya hivyo katika mashirika mengi na hili la Tanesco siyo tukio la kipekee.”

“Binafsi sijawahi kuwa na mawasiliano ya aina yeyote na uongozi wa Tanesco, kushawishiwa juu ya hatua ambazo POAC ndiyo imezichukua za kutaka kujiridhisha juu ya utaratibu waliotumia.”
“Ieleweke wazi kabisa kuwa hakuna wakati wowote, popote ambapo mimi au kamati yetu imekataa Mkurugenzi Mkuu wa Tanesco kuchunguzwa kwa tuhuma zozote. Ambacho tumesisitiza wakati wote ni ufuatwaji wa taratibu, kanuni na sheria, hili nitalisimamia iwe masika au kiangazi.”

Mbunge huyo wa Kigoma Kaskazini kwa tiketi ya Chadema alisema kutokana na imani hiyo, anaunga mkono suala la tuhuma za rushwa zinazotajwa zichunguzwe na Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge kwa kina.

“Nakiomba pia chama changu, Chadema na vyombo vya dola vichunguze tuhuma hizo na kujiridhisha na ninaahidi kushiriki kikamilifu, iwapo nitatakiwa katika uchunguzi wowote utakaofanywa na niko tayari kuwajibika iwapo nitakutwa na hatia yoyote,” alisema.

“Napenda kuwatoa hofu wananchi wa Jimbo la Kigoma Kaskazini walionituma kuja kuwawakilisha hapa bungeni na Watanzania wote kwa jumla kwamba, mimi Zitto Kabwe sina bei, sijawahi kuwa nayo na sitarajii kuwa nayo huko mbeleni.”

“Daima nasimamia kidete maadili ya uongozi bora katika maisha yangu yote ya siasa na ninaahidi, sitarudi nyuma katika mapambano dhidi ya rushwa katika nchi hii pamoja na mikakati ya aina hii ya kunidhoofisha na kunivunja moyo.”

Zitto alilaani kile alichosema kuwa tabia iliyoanza kujengeka katika siku za hivi karibuni ya kuwamaliza wanasiasa wenye kudai uwajibikaji na uzalendo na kuanzishwa kiwanda kwenye medani ya siasa cha kuzalisha majungu na fitina, zenye lengo la kuwachonganisha wanasiasa wa aina hiyo na wananchi kwa kutumia nguvu za fedha.

Awashukia Profesa Muhongo, Maswi
Aliongeza kwamba, akiwa Dodoma amewahi kupata taarifa kwamba Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo na Katibu Mkuu wake, Eliachim Maswi ndiyo wanaosambaza taarifa kwamba amepewa rushwa na Tanesco.

“Hali hii inaniondolea shaka juu ya ushiriki wao katika kueneza au kuthibitisha uvumi huo. “Ninajaribu sana kuzuia kutokuwa na shaka na ushiriki wao huo ikizingatiwa uzito na taswira ya nafasi zao katika jamii, lakini wameshindwa kunidhihirishia tofauti,” alisema.

Mbali na kuwatuhumu watendaji hao wa Serikali kwa kumchafua, Zitto alieleza kushangazwa na kauli zao kwamba mgawo wa umeme sasa basi, akieleza kuwa si kweli.

“Ili kumaliza tatizo la mgawo wa umeme kama alivyosema waziri na katibu mkuu, tunapaswa kuwa na Sh42 bilioni kila mwezi kuzilipa kampuni za IPTL na Symbion kama ‘service charge’, fedha hiyo haijatengwa kwenye Bajeti. Sasa msishangae baada ya wiki mbili mgawo ukarejea na watu watasema hizo ni njama za mafisadi,” alisema.

Zitto alisema waziri pia hakuwa sahihi kueleza kuwa Tanesco inapoteza Sh40 bilioni zinazotokana na mapato yake kwa mwezi baada ya matumizi ya Sh11 bilioni kwa kuwa hadi sasa shirika hilo la umma lina madeni mengi.

“Hivi inawezekana kweli maelezo hayo ya waziri kwamba kila mwezi Tanesco inatumia Sh11 bilioni kulipa mishahara na kupoteza Sh40 bilioni, zinazotokana na mapato yake? CAG yuko wapi na Kamati hii (POAC) iko wapi? Yaani wote sisi tusiyaone hayo ila yeye?,” alihoji.

Akizungumzia madai hayo ya Zitto, Profesa Sospeter Muhongo alisema: “Kila wakati tumekuwa tukizungumza juu ya jambo hilo, lakini hata hivyo, kama mnaweza kuangalia kupima uzito uko pande gani basi andikeni upande huo kati ya mimi na Zitto.”

Alisisitiza kwamba hakuna mgawo wa umeme na hilo ndilo analotaka Watanzania wafahamu na waondoe shaka na kamwe wasitegemee kusikiliza mawazo kutoka kwa watu ambao wanaamini kwa kufanya hivyo watajenga umaarufu.

Maswi hakupatikana jana kuzungumzia tuhuma hizo za Zitto baada ya simu yake ya mkononi kuita muda mwingi bila kupokewa na hata alipoandikiwa ujumbe mfupi hakujibu.

No comments:

Post a Comment