Thursday, June 14, 2012

Kuingiza magari kodi juu & Bia, soda bei juu na sigara!!

SERIKALI imepandisha kodi kwa asilimia 20 kwa magari yanayoagizwa kutoka nje ya nchi, yaliotengenezwa mwaka 2004 kurudi nyuma.

Akizungumza jana bungeni wakati akisoma Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa mwaka 2012/13, Waziri wa Fedha na Uchumi, Dk William Mgimwa alisema magari ambayo yalitengezwa kwa miaka minane iliyopita na zaidi kodi imepanda kwa asilimia 20.

Alisema lengo la hatua hiyo ni kuboresha huduma ya kuagiza magari ili wananchi waache kununua magari kuukuu, lengo likiwa ni kuboresha na kulinda mazingira.

Kutokana na hatua hiyo ya Serikali matarajio ni kwamba bei za magari zitapanda.
Pia katika hotuba hiyo, Waziri huyo alisema kwamba kodi kwa wasafiri wa ndege itaongezeka kwa abiria wanaotoka kwenda nje ya nchi hadi Dola40 za Kimarekeni badala ya Dola30.

Abiria watakaokuwa wakisafiri kwa ndege safari za ndani ambao awali walikuwa wanalipa kodi ya Sh5,000 sasa watalazimika kulipa Sh10,000.

Katika hatua nyingine, Dk Mgimwa ametangaza kodi maalumu kwa namba binafsi za magari, wa Sh5 milioni kwa miaka mitatu.

Alisema lengo la kurekebisha sheria ya kodi ni kukusanya Sh6,360 milioni na kuboresha Pato la Taifa.

Pia...SERIKALI imetangaza mabadiliko ya Sheria mbalimbali zinazohusu kudi, zitakazoathiri bei za bidhaa muhimu nchini kwa lengo la kuongeza mapato ya Serikali.

Akisoma Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka 2012/13, Dk Mgimwa alisema kodi za bia, vinywaji baridi na vinywaji vikali zitapanda kuanzia Julai Mosi mwaka huu.

Katika ongezeko hilo, soda zitapanda kwa Sh14 kwa lita kutoka Sh69 hadi Sh83, bia yenye kimea pekee itaongezeka kwa Sh62 kutoka Sh248 hadi Sh310 kwa lita wakati bia nyingine zitaongezeka kutoka Sh420 hadi Sh525 kwa lita, sawa na ongezeko la Sh105.

Vilevile kodi ya mvinyo unaotengenezwa kwa zabibu zinazolimwa ndani imeongezeka kwa asilimia 75 kutoka Sh145 hadi Sh420, sawa na ongezeko la Sh275 kwa lita.

Kuhusu mvinyo unaotokana na zabibu za nje umeongezwa kodi kutoka Sh1,345 kwa lita hadi Sh1,614 sawa na ongezeko la Sh269 kwa lita.

Vinywaji vikali vimeongezwa kutoka Sh1993 kwa lita hadi Sh2,393 sawa na ongezeko la Sh399.
Bidhaa nyingine iliyoongezwa kodi ni sigara za aina zote, ambazo zile zisizo na kichungi zinazotumia tumbaku ya hapa nchini, imepanda kutoka Sh2,820 hadi 8,210 kwa sigara 1,000.

Wakati zile zenye kichungi na tumbaku ya ndani zimeongezwa kutoka Sh16,114 hadi 19,410 kwa bunda; wakazi zile nyingine zikipanda kutoka Sh29,264 hadi Sh35,117 kwa bunda.

No comments:

Post a Comment