Sunday, June 17, 2012

Ufisadi watikisa UDOM.......


  Ada Bodi ya Mikopo zadaiwa kutafunwa.......

Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) kwa kushirikiana na benki moja mjini hapa kinadaiwa kujihusisha na ufisadi wa kutafuna ada za wanafunzi wanaolipiwa na Bodi ya Mikopo (Heslb).

Wanafunzi wanaolipiwa ada na bodi hiyo walilalamika kupitia gazeti hili kuwa wamegundua ufisadi huo wakati walipofika chuoni hapo kuchukua vyeti vya shahada baada ya kuhitimu chuoni hapo mwaka jana.

Kwa ujanja huo wanadai wanalipa ada licha ya kwamba bodi imewalipia hivyo kuwaneemesha mafisadi wachache waliobuni mpango huo wa kujitajirisha.

Walidai kuwa licha ya kulipiwa ada na Heslb na wao kulipia kiasi cha asilimia walizopangiwa wanalazimishwa kulipa tena ada kwa maelezo kuwa hakuna rekodi zinazoonyesha kuwa walilipiwa ada na bodi. Hata hivyo, uongozi wa chuo cha Dodoma umepinga madai yao.

“Tulichogundua ni kwamba bodi imetulipia mikopo lakini UDOM ama taarifa zimefichwa, au zimepotezwa kwa makusudi ili kutulipisha mara mbili. Tumefuatilia bodi lakini nako wanatuambia tumewalipia chuo kimechakachua,” alisema mwanafunzi aliyeathirika, jina linahifadhiwa.

Walidai kuwa baada ya kuchunguza walibaini kuwa pesa hizo zimepokelewa UDOM lakini ujanja unafanywa kwa kushirikiana na wafanyakazi wa benki moja (jina tunalo) ambao hupitisha fedha hizo na kufuta rekodi za waliolipiwa chuoni ili kuharibu ushahidi wa taarifa za malipo.

Walidai kuwa ujanja wa kula fedha za wanafunzi unafanywa kwa kila idara na kozi ambapo malipo hufanywa kwa kuruka simesta (muhula) mmoja mmoja kwa takribani kila mwanafunzi ili kuwachanganya wanafunzi ambao wanakosa pa kuanzia.

Wanafunzi hao walitoa nakala ya Meneja wa Kanda wa Heslb , Chikira Jahari ya Juni 11, 2012 iliyotoa taarifa za mikopo yao kulipwa na bodi lakini walipofika chuoni waliambiwa hawajalipiwa.

“Hata tuliporudi bodi tulikosa msaada maana tuliambiwa pesa zimewasilishwa UDOM ambako nako tuliambiwa bodi haijalipia,” alidai mwanafunzi aliyeathirika.

Akitoa ufafanuzi, Makamu Mkuu wa Chuo anayeshughulikia taaluma chuoni hapo, Profesa Ludovick Kinabo, alipinga madai yao kwa maelezo kuwa wanaolalamika ni wale waliochukua pesa za bodi lakini hawataki kulipa ada.

Alisema madai ya kuficha taarifa za mikopo ya wanafunzi si ya kweli kwani ukaguzi wa ndani umefanyika lakini haukubaini kukosekana kwa taarifa hizo za fedha.

Aliwataka wanafunzi hao kuacha kuficha ukweli kwani baadhi yao wanataka kuchukua vyeti bila ya kulipa ada jambo ambalo chuo hakiwezi kulikubali.

Wanafunzi hao walituhumu uongozi wa chuo kuwa umejaa udini na siasa na kwamba kuna urasimu unaokwamisha maendeleo ya taaluma hadi uendeshaji wa shughuli za kila siku. Walitaka Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Serikali kufuatilia ufisadi chuoni hapo.

Pia walikilaumu chuo kwa kufukuza wanafunzi wanaodaiwa kuwa walikishabikia chama kimoja cha siasa. Walidai kuwa siku ya tukio wanafunzi hao walikodi mabasi kwenda kusikiliza hotuba za viongozi wa chama hicho, lakini magari hayo yalilazimishwa kwenda ofisi za utawala chuoni hapo kukaguliwa.

“Magari yalipofika utawala uongozi ulichukua vitambulisho vya wanafunzi na kuorodhesha majina kisha kuwafukuza wote kwa kutumia sababu mbalimbali zilizotungwa na uongozi,” alidai mwanafunzi mmoja.

NIPASHE iliwasiliana na Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi, Philipo Mulugo, ambaye aliahidi kufuatilia suala la bodi ya mikopo na kulitolea ufafanuzi.....

No comments:

Post a Comment