CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) jana kiliteka jiji la Dar es Salaam kilipofanya mkutano mkubwa wa hadhara katika Viwanja vya Jangwani kwa lengo la kuzindua mkakati wake mpya unaojulikana kama ‘Movement For Change-M4C’ (Harakati za kuleta mabadiliko) ukiwa na lengo la kukiandaa chama hicho kuongoza dola mwaka 2015.
Katika mkutano huo uliohudhuriwa na maelfu ya wakazi wa jiji la Dar es Salaam na vitongoji vyake, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe aliwaonya watu aliowaita wasaliti ndani ya chama hicho, kwa kuwataka wajirudi mara moja, vinginevyo watashughulikiwa kwa mujibu wa taratibu.
Hivi karibuni Mbunge wa Maswa Magharibi, John Shibuda amekuwa akizozana na viongozi wa chama hicho tangu pale alipotangaza nia yake ya kuwania urais huku akimtaja Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete kuwa atakuwa meneja wake wa kampeni. Bila kumtaja jina, Mbowe alianza kwa kutoa kauli zilionekana moja kwa moja kumjibu Shibuda, akisema wapo watu wanaodai kuwa Chadema ni chama cha udini na ukabila na kusisitiza kuwa huo ni uzushi.
Wakati akiendelea kusema hayo, umati uliokuwepo uwanjani hapo ulipokea kauli hiyo kwa kupaza sauti kwamba “Shibuda ang’olewe …Shibuda ang’olewe… Shibuda aondoke!’ hoja iliyojibiwa na Mbowe papo kwa hapo kwamba mkutano huo haukuwa na lengo la kumng’oa mtu.
“Sikuja hapa kumng’oa mtu…Tumng’oe?” Alihoji Mbowe na kuongeza: “Ngoja nitoe kauli ya chama. Chama chetu hakitayumbishwa na mtu yeyote msaliti. Tutatumia vikao vya chama. Tuzungumze mambo yenye maslahi ya taifa, siyo mtu mmoja mwepesi. Kama mtu hajui moto auchezee.” Alisisitiza kuwa chama hicho kimejengwa kwa zaidi ya miaka 20 na kimeweza kujenga ngome katika mikoa ya Mwanza Lindi na Mtwara. Huku akinukuu kauli ya Rais mstaafu wa Afrika Kusini, Nelson Mandela aliyoitoia miaka ya 1960, Mbowe alilitaka Jeshi la Polisi kutowatisha wanachama wa Chadema na kuonya kuwa wakifanya hivyo, wananchi nao watajibu mapigo. “Chadema kitakuwa chama cha mwisho kuvuruga amani nchini. Nawaonya kama Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni na kama Mwenyekiti wa Chadema na kama Mbunge. Nawaomba polisi, waache kuwasumbua wana Chadema,” alionya Mbowe. Licha ya Jeshi la Polisi kuzuia maandamano ya wanachama wa chama hicho kikuu cha upinzani, watu walianza kufurika katika Viwanja vya Jangwani kuanzia saa 8:00 mchana. Kampeni ya Movement for Change(M4C) Akizungumzia mkakati huo, aliwataka wanachama wa Chadema na wananchi kwa ujumla kujitolea kukichangia fedha ili kufanikisha kampeni hiyo kwani alisema kukiondoa CCM madarakani si kazi rahisi, inahitaji gharama kubwa.
“Kila mwananchi anawajibu wa kubadilisha maisha yake. Kila mtu anapaswa kuwa wakala wa mabadiliko. Kuiondoa CCM kuna gharama kubwa, kule Arumeru watu walichanga kile walichokuwa nacho kuanzia Sh. 50 na kuendelea na tulishinda, au siyo? Tusije tukapata viongozi kwa fedha chafu,” alisema. Mbowe pia alisisitiza kuwa watakuwa makini na wanachama wa CCM wanaohamia Chadema akisema kuwa watatakaswa kwanza kabla ya kupewa uanachama. Kama hiyo haitoshi, chama hicho ‘kilitembeza bakuli’ kwenye mkutano huo, ambapo watu walichanga fedha kwa ajili ya kukisaidia katika utekelezaji wa mkakati huo ambao utafanyika nchi nzima. Awali, Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu, aliwapa somo wananchi kuhusu mchakato wa kuandikwa Katiba mpya. Alisema kuwa katiba ya sasa ni mbovu na kwamba inatakiwa ipatikane mpya ambayo haitachakachuliwa kwa ajili ya maslahi ya Watanzania huku akihoji mfumo wa utawala na suala zima la Muungano wa Tanganyika na Zanzibar. “Je, kuna nchi ngapi katika Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, kuna Amiri Jeshi wangapi katika Jamhuri hii? Hivi hii ni nchi moja au tunataka kuwa na katiba itakayojibu haya yote?” Alihoji Lissu. Aliwataka wananchi kuhoji Tume ya Kukusanya Maoni ya Katiba mpya kuhusu masuala hayo kwa kuwa Katiba mpya ya Zanzibar, inakinzana na Tanzania Bara na kwamba imefumua dhana nzima ya Muungano. “Watanzania wanatakiwa kupewa mamlaka ya kuamua kwa kupiga kura ya maoni ili kuona kama kuna haja ya kuwepo kwa Muungano au kuendelea na hiki kiini macho,” alisema Lissu. Alisema kuwa hata Bunge la Katiba ambalo litaundwa kwa ajili ya kujadili rasimu ya katiba itakayoandaliwa na Tume ya Katiba, linaweza kuchakachuliwa kwa kuwa na wabunge wengi wa CCM ambao watapitisha baadhi ya vipengele kwa maslahi ya chama hicho. “Kwa mtindo huu hatutapata Katiba mpya, yatakuwa yale yale, Sheria ya Marekebisho ya Katiba inatakiwa kufanyiwa marekebisho ili wabunge wa Bunge la Katiba wachaguliwe na wananchi” alisema Lissu. Alisema kuwa sheria hiyo inaeleza kuwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) ndio itakayosimamia kura za maoni na kwamba hali hiyo haitaleta Katiba mpya kwa kuwa Nec imegeuka kuwa Tume ya Taifa ya Uchakachuaji. Aliwataka wananchi kuhoji mamlaka aliyonayo rais kwa kuwa katiba ya sasa inampa mamlaka makubwa kiongozi huyo mkuu wa nchi ambaye anaweza kuamua lolote analotaka. “Inatakiwa kuwe na mfumo wa utawala utakaowapa nguvu wananchi,” alisema Lissu na kufafanua, “ Bunge limejaa zaidi ya wabunge 100 ambao hawajachaguliwa na wananchi, hivyo kazi yao ni kugonga meza tu, jengeni hoja zitakazoingizwa katika katiba mpya ikiwa ni pamoja na kulifanya Bunge kuwa na mamlaka ya kuiadabisha Serikali na ikiwezekana hata mkuu wa nchi”. Lissu alimataka Rais Kikwete kuheshimu ahadi aliyoitoa kwa viongozi wa Chadema waliokwenda Ikulu kupeleka maoni ya chama hicho kuhusu katiba. “Rais alitueleza wazi kuwa atafanyia marekebisho sheria ya mabadiliko ya Katiba kwa kuwa tuliilalamikia kwamba haikuwa sawa, ila naona hakuna alichokifanya, tunamuomba aheshimu ahadi yake,” alisema Lissu. Kwa upande wake Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk Willbroad Slaa ambaye tofauti na ilivyozoeleka, hakuzungumza kwa muda mrefu. Aliwataka wabunge wa chama hicho kuzungumzia matatizo yanayowakabili wananchi watakapokuwa bungeni mwezi ujao. “Maisha ya Watanzania si mazuri, vyakula vinauzwa kwa bei kubwa…, nitatumia nafasi hii kuwaeleza machache wabunge wangu ili wakayaseme bungeni, wabunge wetu hawana wa kuwafunga mdomo, maisha yanazidi kuwa magumu lakini yamekuwa mazuri kwa mafisadi, ”alisema Dk Slaa. Alisema kuwa Serikali inatakiwa itumie kodi ya wananchi kwa ajili ya shughuli za maendeleo na sio kuwalipa watumishi ambao nafasi zao hazina manufaa kwa wananchi. “Kuongeza kodi katika mafuta ya taa ili watu wasichakachue mafuta ya dizeli ni mwiba kwa Watanzania…, hii ni sawa na hoja ya mwendawazimu, wanatakiwa kudhibiti uchakachuaji sio kupandisha bei,” alisema. Dk Slaa pia aligusia mchakato wa Katiba mpya akiwataka wananchi kutoa maoni yao kuhusu mamlaka makubwa ya rais kwa kuwa ndio yanayochangia ugumu wa maisha kwa Watanzania. “Inakuwaje rais anateua mawaziri 55 halafu wananchi wanashindwa kuhoji, Uingereza mawaziri wapo 20 tu,” alisema Dk Slaa. Shamra shamra mkutanoni
Mbowe, Katibu wake Dk Slaa, wabunge na viongozi wengine walifika katika viwanja hivyo saa 9:30 na kufanya umati mkubwa uliokuwepo eneo hilo kulipuka kwa shangwe. Wabunge waliotia fora katika mkutano huo ni pamoja na Mbunge wa Ubungo John Mnyika tangu alipoingia uwanjani hapo na hata alipopewa nafasi ya kusalimia alishangiliwa kwa nguvu. Mnyika ambaye hivi karibuni alishinda kesi yake ya ubunge iliyofunguliwa na mpinzani wake kutoka CCM Hawa Ngh’umbi, alisema kesi hiyo imedhihirisha kuwepo kwa mfumo mbovu wa uchaguzi na kwamba madai yake kwamba CCM kimekumbatia mafisadi ni ya kweli. Aliyekuwa Mbunge wa Arusha mjini Godbless Lema naye alishangiliwa kwa nguvu hasa pale aliposema ni heri kuwa na vita vya kudai haki kuliko kuwa na amani inayopumbaza. Mkutano huo pia ulihudhuriwa na vyama marafiki kutoka nchi 16 za Afrika na baadhi ya viongozi kutoka chama tawala cha Ujerumani cha CDU. Chadema pia kiliendesha kampeni za ‘Vua gamba vaa gwanda’ ambapo kilivuna wanachama wapya 3,120 waliorudisha kadi zao wengi wakitoka CCM. Awali Chama cha CDU kiliendesha semina kwa viongozi wa Chadema kuhusu matumizi ya vifaa vya elektroniki katika masuala ya uchaguzi.
No comments:
Post a Comment