VIJANA WAMBANA, WATAKA AHAMIE CHADEMA, MWENYEWE AWASHAURI WAWE NA SUBIRA....
WAZIRI Mkuu aliyejiuzulu, Edward Lowassa amesema Chama Cha Mapinduzi (CCM), kina tatizo la uongozi na utendaji lakini licha ya kasoro hizo ametaja mambo matano yanayomfanya aendelee kuwa mwanachama wake.Mbunge huyo wa Monduli (CCM), alisema moja ya jambo hilo ni misingi yake ya awali likiwamo suala la kutetea wanyonge.
“Siku CCM inaacha kutetea wanyonge mimi si mmoja wao,” alisema juzi huko Mto wa Mbu, Monduli mkoani Arusha alipokuwa akizungumza katika mkutano wa hadhara.
“Pamoja na uzuri wake, muundo wa chama chetu ni mzuri sana, imani ya chama chetu ni nzuri sana, misingi inayoongoza chama chetu ni mizuri sana, lakini tuna tatizo la utendaji na uongozi ndani ya chama chetu,” alisema Lowassa na kuongeza:
“…Ama katika kufanya maamuzi, ama kufanya maamuzi yasiyo sahihi au kutochukua hatua kwa matatizo yanayowakabili wananchi kwa wakati muafaka.”
Lowassa alieleza kuwa matatizo hayo ndiyo yanayowafanya watu wakichukie chama hicho na kukiona kuwa ni kero kwao hivyo kutafuta mbadala wake.
Kauli hiyo ya Lowassa imekuja huku Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM (Nec), ikitarajiwa kukutana Dodoma kuanzia wiki ijayo, pamoja na mambo mengine, kitajadili mustakabali wa kisiasa nchini.
Pia hii ni mara ya kwanza kwa Lowassa kukikosoa chama hicho kinachoongozwa na Rais Jakaya Kikwete anayeaminika kuwa mtu wake wa karibu.
“Misingi mitano inayonifanya niwe mwanachama wa CCM, moja ni kwamba ni chama kinachotetea wanyonge. Sababu nyingine ni umoja na mshikamano, msingi wa tatu ni kwamba raia wa kawaida analindwa katika kupata na kufaidi rasilimali za nchi dhidi ya matajiri na wawekaji wa nje. Msingi wa nne na tano ni mfumo unaowezesha watu kujisahihisha... “Ndani ya CCM kuna vikao, kuna taratibu za vikao, kuna kufukuzana, kuonyana, lakini kubwa, kuna haki za msingi za mwanachama za kupiga kura au kupigiwa kura.”
Alisema CCM hakibagui watu kwa mizengwe wala rushwa au kwa hila na hizo ndizo sifa zake tangu uhuru. “Siku tukiihama hiyo (misingi) watatuhama wanachama wengi,” alionya.
Lowassa alisema kitendo cha viongozi kushindwa kushughulikia kero ndiyo mwanzo wa chama hicho kuparaganyika kwa kuwa watu wanatafuta mbadala wa kero zao na matatizo yao.
“Tukionekana hatujali shida za wananchi wetu, watatafuta mbadala, lakini kero hizi zishughulikiwe kwenye vikao,” alisema
Shinikizo kuhamia Chadema
Kauli hiyo ya Lowassa imekuja saa chache baada ya kukutana na kundi la vijana makada wa CCM katika Wilaya ya Monduli ambao walimshinikiza atoe msimamo wake kwa madai kwamba amekuwa akiandamwa na kuonewa ndani ya chama hicho huku wakimtaka ahamie Chadema.
Habari kutoka Monduli ambazo pia zimethibitishwa na watu walioko karibu na kiongozi huyo zinadai kuwa vijana hao juzi walimfuata Lowassa nyumbani kwake na kumtaka atoe msimamo wake kisiasa kuhusu kuhamia upinzani au kubaki CCM.
Vijana hao pia walitumia fursa hiyo kumhakikishia kuwa wataendelea kumuunga mkono na kuwa naye sambamba kwa uamuzi wowote atakaouchukua hata kama ni kuhamia upinzani.
Habari zilizopatikana jana kutoka kwa baadhi ya watu waliohudhuria kikao cha ndani kati ya Lowassa na vijana hao zilieleza kuwa walilalamikia kile wanachodai unyanyasaji, udhalilishaji na maonevu yanayofanywa na viongozi wa CCM na Serikali yake dhidi ya mbunge wao huyo.
“Pamoja na kuhisi mbunge wao Lowassa ananyanyaswa, kuonewa na kudhalilishwa kwa kuzushiwa maneno ya uongo, vijana waliohudhuria pia walimhakikishia kiongozi huyo kuwa watamuunga mkono kwa kumsikiliza na kumfuata kwa lolote atakaloamua au popote atakapokwenda,” alisema mtoa
taarifa wetu.
Vijana hao pia walimtaka Lowassa kutoa msimamo kuhusu wana CCM, wakiwemo baadhi wanaoaminika kuwa wafuasi wake wa karibu kuhamia Chadema.
Huku wakionekana kutoridhishwa na majibu ya Lowassa, vijana hao wanadaiwa kutishia kuhamia Chadema huku wakimshinikiza naye ahamie huko badala ya kuendelea kubaki CCM ambako walidai kuwa heshima, mchango na thamani yake havionekani licha ya kukifanyia mengi mazuri chama hicho na Serikali yake.
Baada ya kusoma hisia za vijana hao, walioonekana kudhamiria walichokuwa wakikisema (kuhamia upinzani), Lowassa alilazimika kutumia busara na muda mwingi kuwasihi kuwa watulivu na kutumia vikao halali vya chama kutafuta ufumbuzi wa matatizo na changamoto yanayokikabili CCM.
“Siyo sahihi kukihama CCM kwa sasa, nawaomba muwe watulivu na kutumia vikao halali vya chama kujadili na kutafuta ufumbuzi wa matatizo na changamoto zinakikabili chama chetu,” Lowassa alikaririwa akiwaambia vijana hao.
Akizungumzia kauli hiyo, mmoja wa vijana aliyehudhuria kikao hicho alisema bado wana imani kuwa itafika siku wao pamoja na Lowassa watahamia upinzani iwapo mambo wanayoyapigania ndani ya CCM hayatafanikiwa.
Lowassa ambaye yuko Monduli, amekuwa na vikao vya ndani na makundi mbalimbali ya wananchi jimboni mwake kuanzia wazee maarufu, viongozi wa mila, wanawake na vijana.
Jana, alitarajiwa kufanya ziara ya kutembelea eneo la Monduli Juu kushuhudia uharibifu uliofanywa na watu kutoka wilayani Arumeru waliovamia na kuchoma moto makazi wa wananchi wilayani Monduli.
Katika ziara hiyo, kiongozi huyo atazungumza na kuwafariji wapiga kura wake waliokumbwa kadhia hiyo. Kwa mujibu wa ratiba ya mbunge huyo, leo atatembelea Meserani ambako hivi karibuni mifugo kadhaa ya wafugaji wa jamii ya Kimasai ilikufa kwa kudaiwa kula majani yaliyopuliziwa sumu.
Tatizo la ajira
Katika hatua nyingine, Lowassa alirejea kauli yake kuhusu ukosefu wa ajira kwa vijana na kusema ni eneo linaloonekana kuwa kero kwa jamii na kufanya chama hicho kionekane tatizo kutokana na kushindwa kulishughulikia.
“Mimi ni mmoja wa wasemaji wakubwa wa jambo hili ila kuna watu wananipinga, lakini kuna tatizo la msingi la kweli la vijana kutokuwa na ajira nchini,” alisema.
Alisema Jumatano wiki hii, alikutana na Rais Mstaafu, Benjamin Mkapa kwenye Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere Dar es Salaam na kwamba Mkapa aliyekuwa akienda China alimwambia:
“Unazungumza habari ya vijana, siyo kwamba ni jobless tu (hawana kazi), bali ni rest less, yaani hawana matumaini. Ni agenda ya msingi.”
Lowassa alisema kutokana na hali ya ajira nchini aliamua kuanza kuonyesha mfano jimboni kwake.
“Nikasema kabla Serikali haijaanza jambo hili kubwa na la msingi, nianze mwenyewe. Nikakusanya pesa, kila kata nikawapa shilingi milioni 10. Mto wa Mbu na Monduli Mjini nikawapa milioni ishirini, ishirini.”
“Nikasema nawapeni, zenu, kopeshaneni, watu mnao waamini mfanye biashara, mjitoe katika umaskini, sitachukua chochote, nawapeni nyie Mto wa Mbu milioni 20, kopeshaneni ninyi vijana.”
Lowassa alisema ametoa fedha hizo ikiwa ni mchango wake katika kuwakwamua vijana dhidi ya wimbi la umaskini lakini akawataka wazitumie vizuri ili zizae matunda yanayokusudiwa... “Mkijikopesha vizuri nitawaongeza,” alisema.
No comments:
Post a Comment