LONDON, England
WAKATI wachezaji wa Manchester City wakitoka nje ya uwanja na kipigo cha bao 1-0 toka Arsenal, Aprili 8, mashabiki wa timu hiyo hawakuamini kama mwezi mmoja mbele wangeweza kuwa kwenye nafasi nzuri ya kuweka historia jirani na kutwaa taji.
Kiwango kizuri walichoonyesha Arsenal kwenye mchezo huo, na kutolewa nje kwa kadi nyekundu kwa mshambuliaji Mario Balotelli, kuliwaacha mahasimu wa City, Manchester United wakiongoza kwa tofauti ya pointi nane na michezo sita ikisalia.
Ni wazi United walikuwa kwenye nafasi nzuri ya kutwaa ubingwa, lakini sehemu ya kumalizia huenda ilikuwa tatizo kwa upande wao, na baada ya yote hayo walijikuta wakipata ushindi mmoja katika mechi nne zilizofuata.
Hiyo ilitoa mwanya kwa City kupanda kileleni mwa msimamo kwa tofauti ya mabao ya kufunga baada ya kupata ushindi wa bao 1-0 mbele ya United Aprili 30 mwaka huu.
Hakuna timu iliyowahi kukosa ubingwa wakati ikiongoza kwa tofauti ya pointi nane kufikia Aprili.
Kocha Alex Ferguson amekutwa kile kilichomtokea farasi aliyejulikana kwa jina la Devon Loch aliyeangua mita 40 kabla ya kuvuka mstari wa mwisho wakati wa mashindano ya Mbio za Taifa za Farasi mwaka 1956.
Ferguson ana mashaka na matokeo hayo ambayo yamethibitisha udhaifu kwenye kikosi chake baada ya sare wasiyotarajia ya mabao 4-4 na Everton April 22 na kutoa mwanya kwa City kusogea zaidi kwa tofauti ya pointi tatu.
United wangeweza kuzoa pointi zote tatu kwenye mchezo dhidi ya Everton baada ya kuongoza 3-1 na kisha 4-2 kwenye Uwanja wa Old Trafford, lakini mwisho wa mchezo walijikuta wakiondoka na pointi moja.
"Nadhani mchezo dhidi ya Everton ulituua," alisema Ferguson. "Tulionyesha kiwango kibovu dakika 10 za mwisho. Kabisa, hatukuwa makini," alisema.
"Ni sahihi kusema historia ya United ni kushambulia muda wote wa mchezo, lakini tulicheza kizembe na hii imeturudisha nyuma, hakuna swali kwenye hilo. Ni mchezo dhidi ya Everton ndiyo uliotuharibia."
Kama City itaweka historia kwa kuwa timu ya kwanza kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu England kwa tofauti ya mabao ya kufunga, basi bila shaka maneno ya Ferguson yatawachoma zaidi wachezaji wake.
"Ni sawa kurejea kwenye vitabu vya historia ya United, lakini kuna wakati ukweli lazima uwe mbele," alisema Ferguson wakati fulani.
"Tulipokuwa tunaongoza 3-1, 4-1 tungetulia kwa idadi hiyo ya mabao. Lakini tuliendelea kushambulia badala ya kusema: 'Siku yetu imekwisha'."
Pamoja na yote hayo, hatua waliyofika United na City imeweka historia ya pekee katika soka la England ambayo inakaribiana na ile ya mwaka 1989 ambapo kulikuwa na ushindani mkubwa Ligi Daraja la Kwanza wakati huo kati ya Arsenal na Liverpool.
Msimu huu pia umekuwa na ushindani mkubwa, kwani mpaka sasa magoli 1,034 yamefungwa, huku zikisalia mechi 10, na kama kutakuwa na magoli 30 Jumapili wakati ligi ikifikia tamati, basi itazidi mabao ya msimu uliopita 1,063.
No comments:
Post a Comment