JESHI la Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, linamhoji mhadhiri wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Ushirika na Biashara Moshi (Muccobs), kwa tuhuma za kukutwa na vyeti vya kughushi vya vyuo vikuu kadhaa kwenye kompyuta yake.
Kukamatwa kwa mhadhiri huyo (jina tunalihifadhi), kumekuja siku chache baada ya Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida), kuibua tuhuma nzito za kuwepo askari 948, kat
ika Jeshi la Polisi na Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) wenye vyeti bandia vya elimu.
Habari za uhakika kutoka Polisi na Muccobs, zinasema tayari kompyuta ya mhadhiri huyo ambayo ilikutwa na sampuli za vyeti hivyo, inashikiliwa na jeshi hilo kitengo cha makosa ya kughushi.
Taarifa hizo zimeeleza kuwa vyeti hivyo ni vya Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine (Saut) Mwanza, Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (Sua) Morogoro na ‘transcript’ za Muccobs.
Kukamatwa kwa mhadhiri huyo, kumekuja pia wakati kukiwepo kwa taarifa za kuzagaa kwa vyeti bandia vya Muccobs hususan ngazi ya stashahada ambavyo vinadaiwa kuuzwa kama njugu na mtandao mmoja ndani ya chuo hicho.
“Maneno yamekuwa mengi sana juu ya kuwapo kwa watu walioajiriwa katika taasisi mbalimbali nchini wakitumia vyeti vyetu, lakini hawajawahi kumaliza hapa kwetu,” alidokeza mhadhiri mmoja wa Muccobs.
Mkuu wa chuo hicho, Profesa Faustine Bee alithibitisha kukamatwa kwa mhadhiri huyo lakini akasema asingependa kulizungumzia jambo hilo kwa undani kwa kuwa linachunguzwa na polisi.
“Siwezi kusema kwa sababu hata hiyo kompyuta inayosemekana ilikutwa na vyeti hivyo, iko mikononi mwa polisi. Mkiwauliza polisi watakuwa na nafasi nzuri zaidi ya kulizungumzia,” alisema Profesa Bee.
Kamanda wa Polisi Mkoa Kilimanjaro anayehamia Mara, Absalom Mwakyoma alipoulizwa jana alisema yuko safarini na kutaka aulizwe kaimu wake, Yusuph Ilembo lakini alipotafutwa alisema hafahamu jambo hilo.
Nahodha aahidi uchunguzi
Katika hatua nyingine, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Shamsi Vuai Nahodha amesema atalifanyia kazi suala la vyeti vya kughushi lililowakumba askari wake.
Alisema hayo alipokuwa akijibu maswali ya waandishi wa habari baada ya kufungua mkutano wa Chama cha Kilimo Vijijini Afrika (Afraca), uliofanyika Dar es Salaam jana.
Nahodha alisema taarifa hizo za vyeti vya kughushi kwa askari wa JWTZ, amezisikia tu kwenye magazeti hivyo atazifuatilia.
“Nitasoma na nitafuatilia, nitalifanyia kazi na kujua ukweli na kama kutakuwa na ukweli wowote tutaushughulikia,” alisema Nahodha.
Wataka Mkuu wa Majeshi, IGP wajiuzulu
Chama cha siasa cha UPDP kimemtaka Mkuu wa Majeshi, Jenerali Davis Mwamunyange na Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Said Mwema na kuwajibika kutokana na sakata la baadhi ya watumishi wao kughushi vyeti.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa chama hicho, Fahmi Dovutwa alisema makamanda hao wameonyesha udhaifu mkubwa.
“Hii ni hatari kubwa hasa kwa usalama wa nchi yetu kama tunakuwa na wanajeshi ambao wameghushi vyeti halafu bado wanaendelea kuwepo kazini,” alisema Dovutwa.
Alisema suala la kutofanya ukaguzi kwa watu wanaowaongoza hadi kufikia baadhi yao kujinufaisha na vyeti bandia kwa miaka mingi ni udhaifu mkubwa kwa ulinzi nchini.
Mwenyekiti huyo alisema hali hiyo inatia shaka kwamba huenda kuna watumishi ambao si raia kwenye sekta nyeti nchini.
Askari hao walibainika kughushi vyeti hivyo wakati wa mchakato wa utengenezaji vitambulisho vya taifa na kusababisha kazi hiyo kushindwa kufanyika kama ilivyokuwa imepangwa.
Kwa mujibu wa Nida, vitambulisho hivyo vilitarajiwa kuanza kutolewa mwanzoni mwa mwezi huu lakini vimekwama kutokana na uhakiki uliokuwa ukifanywa katika fomu mbalimbali zilizokuwa zimejazwa.
Tayari Polisi na JWTZ wametangaza kuanza kufanya uchunguzi wa suala hilo ili kuwabaini wahusika na kuwachukulia hatua.
from www.mwananchigazeti.com
No comments:
Post a Comment