Wednesday, May 30, 2012

Kagasheni asimamisha vigogo wanne Tanapa...


Ni kuhusiana na mauaji ya faru

Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki, ameanza kazi kwa kishindo katika wizara hiyo baada ya kuwasimamisha kazi maofisa wanne wa Shirika la Hifadhi za Taifa (Tanapa) na Serengeti na askari 28 kutokana na uzembe uliosababisha kuuawa kwa faru wawili katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.

Kagasheki ambaye kabla ya mabadiliko ya Baraza la Mawaziri alikuwa Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, akizungumza na waandishi wa habari jana Jijini Dar es Salaam, alisema maofisa hao wamesimamishwa kazi kuanzia juzi yaani Mei 28 mwaka huu ili kupisha uchunguzi dhidi yao tukio hilo utakaofanywa na tume itakayoundwa.

Aliwataja maofisa hao kuwa ni Kaimu Mkurugenzi wa Uhifadhi Tanapa, Justin Hando, Mkuu wa Kitengo cha Intelejensia Tanapa, Emilly Kisamo, Mkuu wa Hifadhi ya Serengeti, Mtango Mtahiko na Mratibu wa Miradi ya Faru Serengeti, Mafuru Nyamakumbati.

Kagasheki aliwataja pia askari 28 wanaolinda doria katika hifadhi ya Serengeti ambao nao wamesimamishwa kuwa ni Askari Mwandamizi Fatael Mtu, Rashid Athuman, Mohamed Athuman, John Fabian, Goodchance Msela, Joseph Darus, Emmanuel Ishalila na Felician Gwangu ambao wote ni askari wa daraja la pili.

Alisema askari wa daraja la tatu waliosimamishwa ni Jafari Hassan, Malale Mwita na John Urio wakati wa daraja la nne ni Majuto Omari, Deogratias Waisiku, Chacha Ndege, Samson Njoghomi, Leonard Kunjumu, Siad Mkamba, Paul Cosmas, Gabriel Ngazama.

Wengine ni Rajab Mangachi, Adam Likarawe, Anodisu Mushumali, John Zimbi, Drigue Shaabani, Rashid Mangandali, Edson Mbyazi, John Mbilizi na Emmanuel Kilawe.

Alisema maofisa na askari hao wamesimamishwa kazi ili kupisha uchunguzi utakaofanywa na tume atakayoiunda kwani wameonyesha uzembe mkubwa kutokana na kutotoa taarifa za kuuawa kwa faru hao wizarani tangu tukio hilo lililopotokea Aprili mwaka huu na badala yake serikali ikapata taarifa hizo kupitia vyombo vya habari.

“Faru wameuawa tangu mwezi Aprili mwaka huu, lakini Tanapa walisema tukio hilo walilijua, lakini hawakutoa taarifa kwa wizara kitu ambacho kinatia shaka kwamba huenda kuna baadhi yao walihusika kwa namna moja au nyingine katika tukio hili,” alisema Kagasheki.

Alisema Tanapa ndiyo wasimamizi wa hifadhi za taifa na kwamba kutotoa taarifa kwa wizara ni tatizo na udhaifu mkubwa wa kiutendaji na kuonya kuwa hataweza kuvumilia kuona vitendo vya aina hiyo vinaendelea katika wizara hiyo.

Kagasheki alisema katika Wizara hiyo jamii imejenga dhana kwamba ni sehemu ambako kuna uchafu mwingi na wanaofanya vitendo hicho hawachukuliwi hatua jambo ambalo alidai chini ya uongozi wake atahakikisha anafuta dhana hiyo kwa wahusika kuchukuliwa hatua mara moja.

“Kumetokea mabadiliko ya mawaziri na sababu ni nyingi, katika wizara hii ya Maliasili na Utalii kuna sura ya wizara imejengeka kwamba kuna uchafu mwingi, wengine wanasema hii ni wizara ya mali za siri wakimaanisha kwamba vitendo vichafu vinafanyika katika wizara, lakini wahusika hawachukuliwi hatua,” alisema Kagasheki.

Alisema tukio la faru kuuawa lazima kuna siri iliyojificha ama kuna baadhi ya waliosimamishwa wamehusika kwa namna moja au nyingine kwani haiwezekani majangili waingie ndani ya hifadhi na kufanya tukio hilo huku watu waliopewa dhamana ya kulinda hifadhi wapo na wamelijua tukio hilo lakini wamenyamaza.

“Hii vita siyo ndogo ni kubwa lakini naahidi tutapambana, maana haiwezekani tukio limetokea mwezi Aprili mwaka huu halafu wahusika wamenyamaza kimya tu hawatoi taarifa, nahisi kuna uhusiano wa tukio hilo na baadhi ya watumishi waliosimamishwa,” alisema Kagasheki na kubainisha kuwa tume itakapomaliza kazi watakaobainika kuwa hawakuhusika hawatachukuliwa hatua.

Faru waliouawa Aprili mwaka huu ni jike mmoja aliyejulikana kwa jina la Sarah na mtoto wake ambapo mizoga yao ilikuwa katika eneo la Hifadhi ya Serengeti bila pembe.

Tukio la kuuawa kwa faru limekuwa la pili naada ya lile la mwaka jana faru mwingine aliyejulikana kwa jina la George (12) maarufu kama ‘Faru wa JK’ aliuawa na baada ya tukio hilo Serikali iliahidi kuimarisha ulinzi wa wanyama hao kwa kutumia vifaa maalum vya mawasiliano ili kufuatilia mienendo yao.

Kuuawa kwa faru mwingine mwezi uliopita kumewashtua baadhi ya wahifadhi wa Tanapa kiasi cha kufanya kuwa la siri kubwa huku watawala wakikwepa kutoa taarifa za suala hilo wizarani.

Kagasheki ameanza kuchukua hatua za kukabiliana na vitendo vya ufisadi katika wizara hiyo, zikiwa siku chache baada ya Rais Jakaya Kikwete kumuondoa aliyekuwa waziri wa wizara hiyo, Ezekiel Maige, katika mabadiliko ya baraza la mawaziri yaliyofanywa Mei 4, mwaka huu.

Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira, ambayo iliwasilisha taarifa yake bungeni katika Mkutano wa Saba ikimtuhumu Maige kushindwa kudhibiti ubadhirifu katika wizara yake kama ulivyobainika katika ugawaji wa vitalu vya uwindaji wa kitalii na usafirishaji wa wanyama hai nje ya nchi.

No comments:

Post a Comment