Sunday, May 27, 2012

Mwakyembe akesha na abiria waliokwama Tazara....

WAZIRI wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe juzi usiku alikesha na abiria zaidi ya 1,000 waliokwama kwa saa 11 katika stesheni ya Shirika la Reli la Tanzania na Zambia (Tazara) jijini Dar es Salaam kutokana treni kukosa mafuta.
Kutokana na tatizo hilo, Dk Mwakyembe ambaye alifika katika stesheni hiyo mara baada ya kuwasili kutoka safarini India, aliahidi kuwashughulikia watendaji wa Tazara waliosabab
isha uzembe huo.
Dk Mwakyembe ambaye ametimiza siku 20 tangu alipoteuliwa na Rais Jakaya Kikwete kuongoza Wizara ya Uchukuzi, alifika eneo hilo baada ya abiria wawili kumpigia simu na kuomba aingilie kati tatizo hilo.
Alifika stesheni katika hiyo saa 4:01 usiku na kukaa mpaka saa 6:30 usiku alipoondoka na hakukuwa na kiongozi yeyote wa ngazi za juu wa Tazara aliyefika kushughulikia tatizo hilo. Akutana na abiria Baada ya Dk Mwakyembe kuwasili na kuingia katika ukumbi wa kupumuzika abiria wanaposubiri kuondoa, wasafiri walimshangilia kwa nguvu mara baada ya kujitambulisha kuwa ni Waziri wa Uchukuzi na amefika kutatua tatizo linalowakabili, ingawa ni usiku akiwa ametoka safarini India.
Abiria hao waliokuwa na jazba walimwelezea waziri huyo kuwa kufika kwake eneo hilo ni uzalendo ambao hawakuutegemea na kutaka awapatie majibu ya chanzo cha tatizo na namna atakavyolitatua.
Awali, Kabla ya kuingia ndani ya ukumbi huo, uliibuka mvutano wa chini kwa chini baina yake na baadhi ya watendaji na wanausalama waliotaka asingie ukumbini kwa hofu ya kufanyiwa vurugu abiria hao waliokuwa na hasiri.
Lakini Dk Mwakyembe aliwataka watendaji wamfungulie mlango ili aingie ndani ya ukumbi kukutana na abiria hao.
Alipofunguliwa mlango, Dk Mwakyemba akiwa ameongozana na baadhi ya wafanyakazi wa mamlaka hiyo waliokuwa zamu, aliingia ndani ya ukumbi na umati wa watu walimzunguka huku kila mmoja akitaka kuwakilisha kilio chake.

Mmoja wa abiria hao alipasa sauti na akisema; “Tunataka uje huku, mpaka muda huu hatujaondoka, hatuelewi chochote, hatujui kama treni itaondoka au hapana, na kama itaondoka itakuwa saa ngapi? Hawa Tazara wanadharau, wanatutesa! Tunaomba uje utusikilize na ueleze kama safari ipo au la”. Dk Mwakyembe aliwatuliza akisema; “Tulieni, tulieni! Nimekuja hapa kwa sababu baadhi yenu wamenipigia simu kunieleza kuwa mmekwama hapa kwa muda mrefu na mnahiji msaada ili muweze kuondoka.
“Mimi ndiye Waziri wa Uchukuzi, nimekuja kujionea mwenyewe na kuchukue hatua. Ninawaahidi hali hii katika kipindi hiki cha uongozi wangu haitajirudia.
Nitahakikisha ndani ya muda mfupi kunakuwa na mabadiliko makubwa.”
Baada ya maelezo hayo, abiria hao walianza kuzungumza kwa mpangilio na kumweleza waziri huyo kuwa kitendo cha treini ya abiria kuchelewa kuondoka bila taarifa yoyote kinawasababisha usumbufu mkubwa.
Mmoja wa abiria hao, Paulo Michael alisema kama hali hiyo haitadhibitiwa inaweza kulipeleka taifa katika hali mbaya kwa kuwa wananchi wamechoka na kukataa tamaa.
“Mheshimiwa hivi sasa wananchi wamekata tamaa, kama watendaji wa mamlaka hii wataendelea kututesa namna hii …alilalamika Michael ambaye alionekana kukerwa na kitendo hicho.
Alisema watu wakiwamo wanawake na watoto, wanateseka kutokana na uzembe wa watu wachache na kwamba, jambo hilo ni hatari kwa usalama wa nchi.
Akijibu hilo, Dk Mwakyembe alisema; “Kuhusu hili nawahakikishia kuwa halitatokea tena katika kipindi changu, natambua mmeumia, lakini nawaahidi kufanya mabadiliko, nipeni muda mfupi.”
Abiria hao waliendelea kupaza sauti wakimtaka waziri huyo kutoondoka eneo hilo hadi watakapoondoka kwa kuwa watendaji hao wanaweza kuwadanganya.

Hata hivyo, Waziri Mwakyembe kabla ya ombi hilo la abiria alikuwa ameahidi kuwa hataondoka eneo hilo hadi treni litakapoondoka.
Dk Mwakyembe pia aliwahoji abiria hao kama kiwango cha nauli wanazolipa kinalingana na ubora wa huduma zinazotolewa.
Katika mazungumzo hayo alibaini kuwa kulikuwa na wanafunzi waliotozwa nauli ya watu wazima jambo alilokemea na kusisitiza kuwa asingependa kuona linaendelea.
Waziri huyo baada ya kuzungumza na abiria waliokuwa wanasafiri kwa daraja la tatu, alikutana na wa daraja la kwanza na la pili ambao wengi wao ni wageni kutoka nje ya nchi.
Baada ya kuingia katika ukumbi wa abiria wa daraja hizo kujitambulisha, wasafiri hao ambao baadhi walikuwa wamelala waliamka na kuhoji maswali juu ya sababu za kuchelewa na kama safari itakuwapo.
Dk Mwakyembe aliwajibu kuwa hali hiyo imetokana na uzembe wa watendaji na kuwahakikisha kuwa safari treni ipo na itaanza muda mfupi ujao.
Huku abiria hao wakimpongeza waziri huyo kwa ujasiri na uzalendo wa kuwatembelea usiku, baadhi yao walitoa kamera na simu zao kupiga picha za kumbukumbu.
Ahidi kutimua viongozi
Dk Mwakyembe aliahidi atawashughulikia watendaji wote wa mamlaka hiyo waliosababisha uzembe huo.
“Kama ingekuwa mamlaka yangu leo ningetangaza vinginevyo, lakini shirika hili linazihusu serikali mbili za Tanzania na Zambia. Hata hivyo, ili kusonga mbele mabadiliko ni lazima,” alisisitiza Dk Mwakyembe ambaye alifika hapo muda mfupi baada ya kurejea nchini, kutoka India.
Alisisitiza uzembe wa watendaji huo umefikia ukomo na aliahidi kufikisha mwenendo mzima wa utendaji wa mamlaka hiyo katika kikao cha Baraza la Mwaziri.

“Nimekuja kujionea mwenyewe hali hii na nimethibitisha kuwa tatizo ni uongozi. Suala hili nitalifikisha katika kikao cha Baraza la Mawaziri,” aliahidi Dk Mwakyembe. Awali Meneja Mkuu wa Tazara Kanda ya Tanzania, Abdallah Shekimweri alimweleza waziri huyo kuwa usafiri umechelewa kutokana na kuchelewa kupata mafuta ya dizeli.
“Tatizo ni mafuta, yamechelewa kupatikana kutokana na kumalizika mkataba baina yetu na kampuni iliyokuwa inatusambazia mafuta na mwenye uamuzi wa kusaini mkataba ni Mkurugenzi Mkuu ambaye hajafanya hivyo hadi sasa,” alisema Shekimweri.

No comments:

Post a Comment