Wednesday, May 30, 2012

Mhasibu Lindi kortini kwa kumjeruhi mkewe kwa pasi...

MKAZI wa Kata ya Wailes katika Manispaa ya Lindi Bw. Mwanzaga Mbowi amefikishwa Mahakama ya Mkoa wa Lindi akikabiliwa na shitaka la kumjeruhi mkewe kwa kumchoma na moto wa pasi.

Bw. Mboi ambaye ni Mhasibu katika Manispaa hiyo alipandishwa kizimbani Mei 28, mwaka huu na kusomewa shitaka lake na Mwanasheria wa Serikali, Bi. Mwahija Ahamadi.


Akisomewa shitaka lake mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama hiyo Bw. Dustan Ndunguru, Mwanasheria wa Serikali alidai kuwa mshitakiwa alitendo kosa hilo Mei 27, mwaka huu, saa 1:30 asubuhi.

Bi. Mwahija alidai kuwa siku hiyo ya tukio huko Wailes iliyopo katika Manispaa ya Lindi mshitakiwa alimjeruhi mke wake wa ndoa Bi. Olifoncia Chembekwa kwa kumchoma na moto wa pasi.

Aliiambia mahakama hiyo kwamba siku na wakati huo mshitakiwa na mke wake kwa pamoja walikuwepo nyumbani kwao na mara kukatokea kidogo mifarakano ambayo ilipelekea mshitakiwa kumpiga na hatimaye kuchukua pasi ya moto na kumuunguza mlalamikaji mkono wake wa kulia na sehemu nyingine.

Mwendesha mashitaka huyo alidai kutokana na kitendo hicho, mshitakiwa alimsababishia mlalamikaji maumivu makali kwenye mwili wake.

Bi. Mwahija aliiambia Mahakama hiyo kwamba kutokana na kitendo hicho mshitakiwa amefanya kosa chini ya kifungu cha 225 Kanuni ya Adhabu Sura ya 16.

Hata hivyo Mshitakiwa alikana kosa linalomkabili na kupelekwa rumande baada ya upande wa mashitaka kupinga dhamana kwa mshitakiwa kutokana na kutopata taarifa ya maendeleo ya mlalamikaji huku kesi hiyo namba 49/2012,itatajwa tena Juni 11, mwaka huu.

No comments:

Post a Comment