MKUTANO wa nane wa Bunge la Jamhuri ya Muugano wa Tanzania unaingia katika wiki ya pili leo, huku kukiwa na kila dalili za kuwapo mjadala mkali wa hotuba ya bajeti iliyowasilishwa bungeni Alhamisi iliyopita na Waziri wa Fedha, Dk William Mgimwa.
Miongoni mwa mambo yanayotarajiwa kuiweka njiapanda Serikali ni suala la deni la taifa ambalo kwa mujibu wa bajeti iliyosomwa limefikia karibu Sh 20.3 trilioni Machi mwaka huu, kwani wabunge wanataka mchanganuo wa jinsi deni hilo lilivyofikia kiwango hicho.
Suala jingine ambalo linaweza kuzua mvutano ni kile wabunge wanachodai kuwa ni ukaidi wa Serikali kutosikiliza mawazo yao miaka nenda rudi kwa kutotenga fedha za kutosha kwa ajili ya maendeleo.
Katika bajeti yake ya 2012/2013, fedha za maendeleo zilizotengwa na Serikali ni asilimia 30, lakini wabunge wanataka kiwango hicho kiongezwe hadi asilimia 35 na matumizi ya kawaida yabakie 65.
Kadhalika bajeti hiyo, Serikali itakuwa na wakati mgumu kutokana na wabunge wengi kunusa ufisadi katika bajeti ya 2011/2012 kutokana na fedha kidogo zilizopelekwa katika wizara na idara za Serikali, ilhali taarifa za mapato ya nchi zikionyesha kwamba fedha nyingi zilikusanywa na Mamlaka ya Mapato (TRA) hadi asilimia 106.
Suala la kutokuwapo kwa uwiano kati ya mapato na matumizi ya Serikali, ndilo liliwasukuma baadhi ya wabunge wa CCM waliohudhuria kamati ya wabunge wa chama hicho Ijumaa iliyopita, kuibua hoja ya kutaka kuchunguzwa kwa mfuko mkuu wa Serikali kwa maelezo kwamba kuna dalili za kuwapo kwa ufisadi.
Uchambuzi rasmi wa bajeti hiyo utaanza kufanywa na Kamati ya Bunge ya Fedha na Uchumi kupitia maoni yake yanayotarajiwa kusomwa na Mwenyekiti wake, Andrew Chenge na kufuatiwa na Bajeti mbadala ya Kambi ya Upinzani, inayotarajiwa kuwasilishwa na Waziri Kivuli wa Fedha na Uchumi, Zitto Kabwe.
Chenge tayari alishasema kwamba, kamati yake imeelewana na Serikali kwa ahadi ya kurekebisha kasoro za kibajeti katika mwaka ujao wa fedha, lakini baadhi ya wabunge wa CCM katika kikao chao Ijumaa, waligeuka mbogo wakitaka marekebisho makubwa yafanywe.
Kadhalika baadhi ya wabunge hao wa CCM waliripotiwa kutohudhuria kikao hicho kukwepa kuwa sehemu ya makubaliano ambayo yangefikiwa na ‘kuwafunga midomo’ wakati wa kuchangia bajeti hiyo wiki hii.
Licha ya kutengwa fedha kidogo, pia wabunge kadhaa wa CCM na wale wa upinzani wanapinga matumizi makubwa ya Serikali na kupuuzwa kwa mpango wa Serikali wa kubana matumizi, hasa kupunguzwa safari za nje na za ndani za viongozi, kulipana posho, makongamano na mikutano.
Wakati wabunge wa CCM wakiendelea na mkutano wao Ijumaa, Mbunge wa Kisesa, Luhaga Mpina alijitokeza mbele ya waandishi wa habari na kutangaza kwamba hataunga mkono bajeti hiyo na kwamba, yuko tayari kufukuzwa ndani ya CCM kutokana na hatua yake hiyo.
Hoja ya Mpina ni kutaka Serikali ifumue bajeti yake na aliahidi kwamba leo ataomba mwongozo wa Spika ili kutoa hoja ya kutaka bajeti isijadiliwe na badala yake Serikali ipate fursa ya kuifanyia marekebisho makubwa, ikiwa ni pamoja kuongezwa kwa fedha za miradi ya maendeleo kutoka asilimia 30 hadi 35 ya bajeti, pia kupunguzwa kwa matumizi yasiyo ya lazima.
Hoja hiyo ya kushauri bajeti kufumuliwa, pia ilijadiliwa katika kikao cha ndani cha wabunge wa CCM, ambapo Mbunge wa Mwibara, Alphaxard Lugola na Mbunge wa Kilindi, Beatrice Shelukindo, ambao waliungwa mkono na wabunge wengine kadhaa, walinukuliwa wakibainisha upungufu mkubwa uliopo ikiwa ni pamoja na fedha kidogo za miradi ya maendeleo.
Katika kikao hicho, pia wabunge hao, walieleza kutoridhishwa na utekelezwaji wa bajeti katika wizara nne, kutokana na kutengewa fedha kidogo, lakini miradi kutotekelezwa kwa wakati kama ambavyo ilikusudiwa.
Wizara ambazo zilitajwa ni pamoja na Nishati na Madini, Uchukuzi, Wizara ya Kilimo Chakula na Ushirika na Wizara ya maji.
“Katika Wizara ya Nishati na Madini kuna miradi ambayo ilipaswa kutekelezwa badala yake, wakati wa kipindi hiki cha mwisho cha maandalizi ya bajeti, zimekwenda kuwekwa nguzo tu, ili kuonyesha kuanza kwa miradi….Sasa jambo kama hili halifai,” Lugola alinukuliwa akisema ndani ya kikao hicho.
Kutokana na umuhimu wa mjadala wa bajeti, tayari wabunge kadhaa walishajiorodhesha kuchangia mjadala hata kabla ya bajeti kusomwa, lakini Naibu Spika, Job Ndugai alisema wiki jana kuwa kanuni za Bunge zinaruhusu wabunge kujiorodhesha kuchangia baada ya kusomwa bajeti.
No comments:
Post a Comment