Friday, June 15, 2012

Mwendelezo wa Vita kati Ya Dogo Janja Na Tip Top Connection.....

Jana na juzi habari ya Dogo Janja kufukuzwa Tip Top Connection imekuwa gumzo. Kila upande wa wanaouhusika kwenye sakata hili, yaani yeye Dogo Janja na Madee ambaye ndiye aliyehusika kumleta Tip Top na kukabidhiwa na wazazi wake baada ya kumtoa Arusha na kumleta Dar es Salaam, unaongea la kwake. Kutokana na kutofautiana kwa maelezo kwa pande hizi mbili mashabiki wameshindwa waamini lipi! Tip Top Connection wanadai kuwa wamefikia uamuzi wa kumrudisha kwao Dogo Janja ambaye jina lake halisi ni Abdul kutokana na mtoto huyo kuwa mtoro shuleni na kulewa sifa. Lakini kwa mujibu wa maelezo ambayo tuliyapata kutoka kwake mwenyewe Dogo ni kuwa Tip Top walikuwa wanamtumia kimaslahi zaidi kwa kumlipa kidogo kutoka kwenye kile anacholipwa kwenye show zake. Mtoto huyo aliyekuwa anasoma kidato cha pili kwenye shule ya Makongo, anasema maisha yalikuwa magumu licha ya kila show aliyofanya kulipwa sio chini ya shilingi milioni moja na yeye kuambulia laki na ushee. Kingine alidai kuwa Madee alimnyang’anya kadi yake ya benki na kwamba msanii huyo mkongwe alikuwa akichukua hela kwenye akaunti bila ridhaa yake. Hata hivyo kwa mujibu wa maelezo yaliyotolewa na Madee kupitia Clouds FM jana kuhusu shutuma hizo, ni kwamba aliamua kuichukua kadi yake kwakuwa aligundua kuwa Dogo Janja alikuwa akitumia fedha hovyo. Hata hivyo kila Dogo Janja alipotaka fedha alimpeleka benki yeye mwenyewe na kuchukua kiasi anachotaka. Mpaka sasa hakuna anayekubali maelezo ya mwenzie na mchezo umegeuka wa kutupiana mpira pasipo mdakaji wa kudumu. Tatizo kwa wengi limekuja kwa meneja wa Tip Top Connection Babu Tale ambaye namna alivyolipokea tukio hilo limewapa wasiwasi watu wengi. Babu Tale amezipokea shutuma hizo kwa hasira na taharuki na kuahidi kuchukua maamuzi mazito yasiyostahili kufanywa kwa mtoto ambaye hajafikisha hata miaka 18. Amesema kinachofuata ni kuzifuta nyimbo zote za Dogo Janja alizozirekodi akiwa chini ya Tip Top Connection. Babu amedai kuwa Dogo Janja hana shukrani licha ya Madee aliyemtoa kwao ambako wazazi wake walishindwa kumsomesha na kuamua kugharamikia kumlipia ada katika sekondari ya Makongo, lakini leo hii anamshutumu kumdhulumu na kumnyanyasa. Kama kweli Babu Tale ataamua kuzifuta nyimbo za Dogo Janja kama njia ya kulipiza kisasi cha kulichafua jina la familia hiyo, basi ajue kuwa atakuwa amefuta nguvu, jasho na mali iliyotoka kwenye akili ya mtoto aliye kwenye foolish age. Huo ni uamuzi ambao kidogo ungeweza kueleweka kama ungefanywa kwa msanii mwenye umri kama wa kwake Babu Tale. Angeonekana mstaarabu sana kama angesema, “Okay sawa pamoja na kutudhalilisha kiasi hicho sisi hatuna kinyongo njoo uchukue nyimbo zako zote na uendelee kivyako.” “Muulizeni Adam Juma, nilichokifanya Nairobi, video niliyokuwa nimelipia milioni 4 nilimwambia afute kila kitu kwenye kompyuta kwa mambo kama haya haya,” alisema Babu Tale jana. “Babu Tale ukigombana na Dogo Janja ukatumia nguvu kama vile unapambana na Lord Eyez unanisikitisha! Tip Top connection ikishaniambia Dogo aliingiza shilingi ngapi na nyinyi mlimpa shilingi ngapi ndipo tutaelewana!,” ameandika jana mtangazaji wa Clouds FM, Arnold Kayanda. Hamady Abdughalib Iddy akaongeza, “Mb Dog , Keisha,Cassim, hawa ni baadhi ya wasanii waliokimbia unyonyaji pale Tip Top. Hawa jamaa ni matapeli ni mwisho yaani kama Madee kumlipia mtoto ada ndio anachukulia advantage ya kumnyonya inasikitisha sana.” Kwa maoni hayo juu ni wazi kuwa lawama nyingi sasa zinaelekezwa kwa Tip Top Connection na kwa uamuzi kwa ‘moto kwa moto’ ama ‘jino kwa jino’, hawatafika popote zaidi ya kundi hilo kuchukiwa na kila mtu. Babu Tale na uongozi mzima utambue kuwa wanataka kujiingiza kwenye vita na mtoto mdogo ambaye bado anastahili kukalishwa chini na kuambiwa, sio kwa kumpiga kama ambavyo wanataka kufanya ili kumharibia maisha yake kama msanii.

No comments:

Post a Comment