Friday, June 1, 2012

Kortini kwa kukutwa na risasi za SMG uwanja wa ndege!!!

MFANYABISHARA na Raia wa China, Jiaw Liu jana alifikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Ilala kujibu shtaka la kukutwa na begi la Risasi katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere jijini Dar es Salaam.

Liu ambaye ni mkazi wa Upanga Magharibi alifikishwa mahakamani juzi kujibu shtaka la kukutwa na begi lililokuwa na risasi za bunduki aina ya SMG kinyume cha sheria.

Mwendesha Mashtaka Munde Kalombola alidai mshtakiwa alitenda kosa hilo Mei 27mwaka huu, katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere uliopo jijini Dar es Salaam. Kalombola alidai siku ya tukio saa 9;00 alasiri katika uwanja huo, mshtakiwa alikamatwa akiwa na begi lililojaa risasi za bunduki aina ya SMG yenye namba 352 bila ya kuwa na leseni ya umiliki.

Mshtakiwa alikiri shtaka na hakimu Pamela Kalala aliahirisha kesi hiyo hadi Juni 11,mwaka huu itakapotajwa tena. Mshtakiwa kwa sasa yupo nje kwa dhamana baada ya kutimiza masharti ya dhamana ya kuwa na wadhamini wawili wa kuaminika ikiwemo kuwasilisha hati yake ya kusafiria mahakamani hapo.

Pia mshtakiwa huyo hatakiwi kusafiri nje ya nchi mpaka kesi yake itakapomalizika . Katika hatua nyingine, Mkazi wa Mtongani jijini Dar es Salaam, Penina Mlayi (23) alifikishwa katika mahakama hiyo kujibu shtaka la kujaribu kujiua.

Mwendesha Mashtaka wa serikali Sakina Sinda alidai mahakamani hapo kuwa mshtakiwa alitenda kosa hilo Mei 11, mwaka huu katika hospitali ya Aga Khan.

Sinda alidai siku ya tukio saa 11:00 jioni katika Hospitali hiyo mshtakiwa alijaribu kujiua.
 Mshtakiwa alikana shtaka na hakimu Wilberforce Luhwago aliahirsiha kesi hiyo hadi Juni 11,mwaka itakapotajwa tena. 
Hadija Jumanne

No comments:

Post a Comment