Mada yetu ya leo Jumamosi , tutaeleza kwa kina jinsi uvuvi haramu unavyofanyika kwatika maeneo ya karibu na fukwe za Bahari ya Hindi jijini Dar es Salaam.
Leo tukiangaza athari za kimazingira zinazosababishwa na uvuvi huu wa kutumia baruti pia athari za kiafya wanazoweza kuzipata walazi wa samaki hawa.
Daktari bingwa katika Chuo Kikuu cha Sayasi za Tiba, Muhimbili, Henry Mwakyoma, anaweka wazi kuwa, samaki hao huweza kusababisha saratani na maradhi ya figo.
Dk Mwakyoma anasema, mwili wa samaki hufyonza sumu yote iliyoko katika bomu lile mara baada ya kupigwa na kwamba sumu hiyo huweza kupita aidha katika nyama au mapafu yake. “Sumu inayoingia mwilini mwa samaki inategemeana na mchanganyiko uliotumika kutengeneza bomu hilo,” anasema Dk Mwakyoma.
Kwa bomu lililotengenezwa kwa mbolea ya chumvichumvi, mafuta ya taa, baruti, na dongo au ‘waterexplosive gel, daktari anathibitisha kuwa na sumu kali na husababisha maradhi ya saratani na figo.
“Endapo mtu atakula samaki wa aina hiyo mara kwa mara, anakuwa kwenye hatari kubwa ya kupata maradhi ya saratani na figo,” anasema mtaalamu huyo.
Dk Mwakyoma anaongeza kuwa, bidhaa kama mbolea ya chumvichumvi na baruti ni sumu hatari kwa mwili wa mwanadamu hata kama samaki huyo atakuwa amepikwa.
“Kwa sababu samaki ana nyama laini, hupikwa kwa muda mfupi, na hivyo sumu ile hubaki katika nyama ikiwa na nguvu,” anafafanua Dk Mwakyoma.
Anasema, samaki wa aina hiyo anapoliwa huchukua muda mrefu kiasi kwa madhara yake kuanza kuonekana kwa binadamu kwa kuwa utengenezaji wa mabomu hayo ya kienyeji, wakati mwingine hutumia mbolea za viwandani na baruti.
Samaki wa mabomu
Wataalamu wa masuala ya uvuvi, wanasema, samaki aliyevuliwa kwa mabomu hutambulika kwa urahisi.
Mishipa ya damu iliyoko katika matamvua ya Samaki aliyevuliwa kwa mabomu hupasuka hivyo huvilia damu na kupata rangi nyekundu.
Dalili nyingine ni utumbo wake kusagika na kutawanyika, bandama kupasuka na mwili wa samaki huyo huacha tundu unapobonyezwa hata kwa kidole.
Akizungumza na gazeti hili Waziri wa Mifugo na Uvuvi, David Mathayo alikiri kuwepo kwa watu wanaonunua vifaa vya kutengeneza mabomu kwa visingizo vya kulipulia miamba.
“Tukipata majina yao,watashughulikiwa mara moja, lakini ukiishutumu idara yote ya uvuvi, utakuwa umekosea,” alisema.
Athari za kimazingira
Watalaamu wa Mamlaka ya Uvuvi (Fisheries) wanasema kuwa, uvuvi wa kutumia mabomu unaathiri kwa kiasi kikubwa mazalia na malisho ya samaki ambayo kitaalamu yanaitwa ‘Coral Reef’.
Festo Mtanga ambaye ni Ofisa Uvuvi kutoka Idara ya Uvuvi ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi, anasema mabomu na baruti huathiri chanzo kikuu cha mazalia ya samaki. Anasema utengenezwaji wa mabomu haya kienyeji ndicho chanzo cha uharibifu mkubwa wa mazali ya samaki kutokana na uwezo wa zana zinazotumika kutengeneza mabomu husika.
“Mabomu yanayotumika sasa ni yale yanayotumika vitani, kubomoa majengo ama madaraja, tofauti ni moja kwamba haya yanatengenzwa. Lakini yakipigwa kwenye matumbawe huharibu kabisa makazi ya samaki,” anasema.
Mtaalamu huyu wa uvuvi, anazungumzia athari za uvuvi haramu kwamba baada ya mazalia ya samaki na viumbe hai kuteketezwa, huchukua miaka 70 hadi 100 kujijenga upya, hali ambayo hukaribisha ujwangwa baharini.
Anasema, mlipuko wa mabomu wakati wa uvuvi, huua viumbe hai vyote na mayai yake na kupoteza kizazi kikubwa cha samaki baharini, mmomonyoko wa fukwe unaosababisha kukosekana kwa vizuizi vya mawimbi, upotevu wa samaki wengi ambao mara nyingi ni vigumu kuwaondoa wote.
Makazi ya samaki
Samaki wanaotaga na dagaa hupendelea kujificha maeneo hayo kwa ajili ya kukwepa samaki wakubwa ambao huwafanya mlo.
Makazi haya mara nyingi huwa yamefunikwa kwa mawe madogo madogo na huwa na chakula cha kutosha na chenye virutubisho kwa samaki. Aidha, kuharibiwa kwa makazi ya samaki, huambatana na kupotea kwa mayai, samaki wadogo na makazi yao.
Hili huathiri kizazi cha samaki kwa kiasi kikubwa na kusababisha upungufu wa maliasili hii. Uvuvi haramu ni ule unaofanyika bila kufuata Sheria na Kanuni za Uvuvi zinazosimamia raslimali za uvuvi kitaifa na kimataifa.
Uvuvi huu unajumuisha kuvua bila kuwa na leseni, kufanya shughuli za uvuvi katika maeneo yasiyoruhusiwa, kuvua kwa zana zisizokubalika kwa mfano kuvua kwa baruti na sumu, Vilevile kuchakata mazao ambayo hayakuvuliwa kihalali na kufanya biashara ya mazao ya uvuvi ambayo yamevuliwa kwa kutozingatia taratibu zilizowekwa.
Pamoja na mabomu, zana nyingine ambazo hutumika kufanya uvuvi haramu ni nyavu zenye macho madogo, nyavu za timba, kokoro, sumu na baruti.
Maisha ya wavuvi
Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Sosholojia cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Huruma Sigalla ambaye alifanya utafiti kuhusu soko na maisha ya wavuvi katika pwani ya Afrika Mashariki anasema, ipo haja ya kuangalia maisha ya wavuvi kwanza kabla ya kuwalaumu kwa kufanya vitendo hivyo haramu.
“Si kwamba tunahalalisha uvuvi haramu, hapana, lakini tunatakiwa tuangalie sababu za watu hao kufanya hivyo,” anasema Dk Sigalla.
Anasema, maisha ya wavuvi wengi ni magumu. Wengi wao hawana elimu, hawana ajira nyingine zaidi ya uvuvi na hicho ndicho wanachokitegemea kuwaingizia kipato.
Hali kadhalika anasema, maeneo ya pwani yana ongezeko kubwa la watu, jambo ambalo linazidisha ukali wa maisha katika ukanda huo.
“Watu wanaongezeka siku hadi siku, samaki wanapungua, mahitaji ya samaki yanaongezeka, ndiyo maana wavuvi hufikia hatua ya kufanya uvuvi haramu,” anasema.
Lakini pia, Dk Sigalla anasema, wavuvi hufikia kufanya vitendo hivyo kwa sababu wanaona kuwa, wavuvi haramu ‘mapapa’ hawachukuliwi hatua.
“Kama wao wanashudia meli kubwa kubwa kutoka China zinakuja, zinavua, nao wanaona ni bora watumie zana hatari kwa ajili ya kujipatia kipato,” anasema.
Anaongeza kuwa, licha ya samaki kuliingizia taifa mapato ya kutosha, lakini bado maeneo ya pwani yapo nyuma kimaendeleo ukilinganisha na mengine.
Aidha, utafiti wa Dk Sigalla ulibainisha kuwa,kuna kesi za wavuvi kufa maji ambazo hazijaripotiwa. “Tumezungumza na wavuvi na wakaweka wazi kuwa, wenzao hufa maji mara kwa mara waendapo katika uvuvi, jambo ambalo linatishia maisha ya kundi hili,” anasema.
Anasema, serikali haina budi kuistawisha sekta hii kwa kuweka taratibu za kujua idadi ya wavuvi wanaokwenda baharini na kuwapa vitendea kazi bora.
“Lakini pia, wanahitaji elimu ya uvuvi salama, nyenzo na uwekwe utaratibu wa kujua wamekwenda kuvua wavuvi wangapi na wamerudi wangapi,” anasema
( Hivi ndivyo vifaa vinavyotumika kutengeneza bomu, mbolea ya chumvi, dongo, utambi na kibati)
No comments:
Post a Comment