NI MAASKOFU, MASHEHE, WASEMA WIZI UPO KWENYE MISAMAHA YA KODI, MAGENDO....
KAMATI ya Viongozi wa Dini, imetoa ripoti yake ya utafiti kuhusu uchumi wa nchi na kusema Serikali inapoteza Sh1.7trilioni kutokana na ukwepaji kodi, misamaha ya kodi na utoroshwaji wa mali na fedha nje ya nchi.
Matokeo ya utafiti wa kamati hiyo yametolewa wakati kesho Serikali inatarajiwa kusoma Bajeti Kuu kwa mwaka 2012/13, huku ikitegemea misaada kutoka nchi wahisani wanaochangia katika Mfuko Mkuu wa Bajeti (GBS). Utafiti huo uliofanywa na Kamati ya Masuala ya Uchumi na Haki za Binadamu (ISCJIC) na kupewa jina la ‘The one billion dollar question: how can Tanzania Stop losing so much tax revenue’ (Suala la dola bilioni moja: Tanzania inawezaje kuzuia upotevu wa kiasi hicho cha kodi?) ilizinduliwa jana jijini Dar es Salaam.
Ripoti hiyo ambayo imetokana na utafiti uliofanywa kwa kutumia nyaraka mbalimbali za Serikali zikiwamo za Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na mashirika ya kimataifa; Benki ya Dunia na Shirika la Fedha Duniani (IMF), imebainisha kuwa Serikali inapoteza Dola za Marekani bilioni moja kila mwaka kutokana na misamaha ya kodi, ukwepaji wa kulipa kodi hiyo na utoroshwaji wa mali na fedha nje ya nchi. ISCJIC inajumuisha viongozi wa Baraza la Kuu Waislamu wa Tanzania (Bakwata), Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT) na Baraza la Maaskofu Tanzania (Tec).
Mtafiti na Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Dk Prosper Ngowi akifafanua kuhusu utafiti huo alisema walitumia vyanzo 167 kupata takwimu hizo na kuwa upotevu uliotajwa kwenye taarifa hiyo wamechukulia ule wa kiwango cha chini zaidi. Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Askofu Paul Ruzoka alisema endapo kiasi hicho cha fedha kingekusanywa, kingesaidia Bajeti Kuu ya Serikali na kuondokana na utegemezi wa fedha za wahisani ambazo mara nyingi huambatana na masharti.
Askofu huyo wa Jimbo Katoliki la Tabora, alisema katika utafiti huo walibaini moja ya mambo yanayochangia upotevu huo kuwa ni sera mbovu za Serikali na uzembe katika ukusanyaji wa kodi. “Ipo haja ya kuwa na mipango mizuri ya kukusanya kodi, kuyadhibiti makampuni yanayotosha fedha na pia kubana kama siyo kuondoa kabisa misamaha ya kodi,” alisema Askofu Ruzoka.
Mwenyekiti huyo wa kamati alisema ni vyema Serikali ikatazama njia nyingine ya kuvutia wawekezaji badala ya kuweka misamaha ya kodi jambo ambalo linawaumiza wananchi. Alisema wakati huu ambao utafiti juu ya upatikanaji wa mafuta na gesi unaendelea, hawana imani kama wananchi watatendewa haki, huku akitolea mfano wawekezaji walio kwenye sekta ya madini jinsi walivyoshindwa kuwasaidia wananchi. Kutokana na hali hiyo, aliwataka wabunge na Serikali kutumia Bunge la Bajeti linaloendelea kujadili jinsi wanavyoweza kukabiliana na hali hiyo.
Ripoti Ripoti hiyo inafafanua kuwa kwa makadirio ya chini, kila mwaka Serikali inapoteza kati ya Dola za Marekani 847 milioni na 1.29 bilioni (Sh1.35 trilioni na 2.05 trilioni), huku akifafanua kuwa makadirio ya kati ni Dola za Marekani 1.07 bilioni sawa na Sh1.7 trilioni.
Kuhusu utoroshaji wa fedha nje ya nchi, alisema baadhi ya kampuni ambazo zina ofisi katika nchi zaidi ya moja, zimekuwa zikitoa taarifa za uongo kuhusu ununuzi wake kwa lengo la kukwepa kodi. Akitoa takwimu ambazo chanzo chake ni Benki ya Dunia (WB) katika ukanda wa Afrika Mashariki, alisema kampuni za Tanzania zinaongoza kwa kutoa taarifa za ukweli.
“Asilimia 69 ya kampuni zilizopo nchini hutoa taarifa sahihi, Uganda ni asilimia 77 na Kenya asilimia 86,” imesema sehemu ya ripoti hiyo... “Kwa maana hiyo, Tanzania ndiyo tunaoongoza kwa udanganyifu lakini wenzetu Kenya angalau wako juu katika kulipa kodi katika mauzo wanayofanya.”
Alisema kampuni 400 ndizo zinazolipa kodi kwa asilimia 70 huku wafanyabiashara ndogondogo wakilipa asilimia 30. “Kampuni kubwa ndizo zinazochangia kwa kiasi kikubwa katika ulipaji wa kodi lakini, kampuni ndogo ni wakwepaji wakubwa wa kodi,” alisema.
Alisema kampuni ndogondogo ndizo zinazoongoza kwa kukwepa kodi kwani ni asilimia 17 pekee ya mauzo ndiyo hutolewa taarifa kwa ajili ya kulipa kodi. Kwa upande wa kampuni ya uchimbaji madini Dk Ngowi, alisema asilimia 65.4 ya kodi inayolipwa na kampuni hizo, inatokana na makato ya kodi kwenye mishahara ya wafanyakazi wake (PAYE).
“Ukiona kampuni za madini zinasema zinalipa kodi ufahamu kwamba zaidi ya nusu ya fedha hizo ni kodi za wafanyakazi, siyo kodi inayotokana na mapato ya madini hayo,” alisema Dk Ngowi. Alisema kodi inayolipwa na kampuni za madini zinazomilikiwa na wawekezaji wa kigeni, zinalipwa na wafanyakazi kupitia kodi ya mishahara yao.
Alisema kampuni ndogondogo ndizo zinazoongoza kwa kukwepa kodi kwani ni asilimia 17 pekee ya mapato ndiyo hutolewa taarifa ili ziweze kulipa kodi. Mhadhiri huyo alipendekeza Serikali itumie utafiti huo kuweka mikakati ya namna ya kupata fedha hizo zinazopotea.
“Fedha hizi zikipatikana tunaweza kuondokana na utegemezi wa misaada kutoka kwa wafadhili,” alisema Dk Ngowi.
No comments:
Post a Comment