Friday, June 1, 2012

JK akubali hoja ya Lowassa..........

 AKIRI TATIZO LA AJIRA KWA VIJANA KUWA BOMU, ASEMA LISIPOTATULIWA LITALETA MACHAFUKO BARANI AFRIKA.

RAIS Jakaya Kikwete amekiri kuwa ukosefu wa ajira kwa vijana ni tatizo kubwa na kwamba lisipotafutiwa ufumbuzi wa kudumu linaweza kusababisha vurugu, machafuko na uasi wa umma, hata kwa nchi zinaoongozwa kwa misingi ya kidemokrasia, kama inavyotokea sasa katika nchi za Kiarabu.



(Rais jakaya Kikwete akizungumza jambo na Rais wa
Ivory Coast,Allasane Wattara katika picha) 

Onyo hilo la Rais Kikwete linafanana na lile ambalo limekuwa likitolewa mara kwa mara na Waziri Mkuu aliyejiuzulu, Edward Lowassa, lakini, linapingana na kauli ya Waziri wa Kazi na Ajira, Gaudensia Kabaka ambaye Machi 21 mwaka huu, alimjibu Lowassa akisema, "Kitendo cha wanasiasa kuendelea kusema tatizo la ajira kwa vijana ni bomu linalosubiri kulipuka, siyo kweli."

Jana akifungua mkutano wa mwaka wa Magavana wa Benki ya Maendeleo Afrika (AfDB) Jijini Arusha, Rais Kikwete alisema moja ya sababu kuu ya machafuko yanayoshuhudiwa sasa kwenye ukanda wa nchi za Kiarabu, ni matokeo ya ukosefu wa ajira kwa vijana na watu kukata tamaa.

“Siyo kweli kwamba machafuko yanayoshuhudiwa kwenye nchi za Kiarabu ni matokeo ya Serikali za nchi hizo kukaa madarakani kwa kipindi kirefu kama wengi wanavyodhani. Ukweli ni kwamba hayo ni matokeo ya ukosefu wa ajira na watu kukata tamaa ya maisha,” alisema Rais Kikwete.

Alisema bila kutafutia ufumbuzi wa haraka, tatizo la ukosefu wa ajira kwa vijana ambao wengi hukimbilia mijini kusaka hali bora ya maisha, hata nchi zenye kuongozwa kidemokrasia, zinaweza kukumbwa na machafuko na uasi wa umma.

Rais alitumia fursa hiyo kuishukuru Denmark kwa kutoa fedha za kusaidia Mfuko wa Ajira kwa Vijana barani Afika, akisema ni moja ya mapendekezo kadhaa yaliyotolewa na kamati maalum ya kutafuta ufumbuzi wa matatizo ya kiuchumi barani Afrika ambayo yeye na Rais wa AfDB, Dk Donald Kaberuka, walikuwa wajumbe.

Mapema Rais wa Ivory Coast, Allasane Ouattara aliyehudhuria mkutano huo aliunga mkono kauli hiyo ya Rais Kikwete kwa kusisitiza kuwa vijana lazima wawekewe mazingira mazuri na kuwezeshwa kukabiliana na kumudu changamoto za kiuchumi, kitamaduni na kiteknolojia wanazokabiliana nazo.

“Lazima wasaidiwe na wawekewe mazingira bora ya kupata fursa za ajira na kujiajiri, bila kufanya hivyo ni kukaribisha matatizo na machafuko yanayotokana na ongezeko la mahitaji na kukata tamaa katika miji yetu inayokua kila kukicha kutokana na ongezeko la vijana wanaosaka ajira na maisha bora,” alisema Rais Ouattara.

Rais Ouattara aliyetumia muda mwingi kumshukuru Rais Kikwete na viongozi wenzake wa Kiafrika kwa kusaidia upatikanaji wa amani nchini mwake alitaja changamoto kadhaa zinazokabili Bara la Afrika, kuwa ni mabadiliko ya tabia nchi, ukame, uhaba wa chakula na ukosefu wa amani kwa baadhi ya sehemu.

Mambo mtambuka
Ili kukabiliana na tatizo hilo, Rais Kikwete alitaja mambo kadhaa yanayopaswa kufanyika ikiwa ni pamoja na kukuza na kuboresha sekta ya kilimo kwa kuongeza uwekezaji na kuacha kutegemea kilimo cha mvua badala yake itumie fursa ya vyanzo vingi vya maji.

“Bara la Afrika linaweza kuzalisha mazao ya kilimo na kujitosheleza kwa chakula na kubakisha ziada ya kuuza nje hadi kuwa ghala la chakula duniani iwapo uwekezaji katika sekta ya kilimo utapewa kipaumbele,” alisema Rais Kikwete.

Kuhusu miundombinu, Rais Kikwete aliipa changamoto AfDB kuongeza juhudi katika ufadhili na udhamini wa miradi ya maendeleo barani Afrika, ikiwemo miradi ya miundombinu aliyosema ni moja ya changamoto zinazokwaza maendeleo ya Afrika.

Alisema pamoja na kukwaza mawasiliano kwa njia ya barabara, reli na anga, uduni wa miuondombinu pia huchangia bei kubwa ya bidhaa na huduma katika nchi za Kiafrika kutokana na gharama kubwa ya usafirishaji.

Rais Kikwete alisema uwepo wa miundombinu ya uhakika siyo tu itawahakikishia wakulima vijijini soko na bei ya uhakika kwa mazao na bidhaa zao, lakini pia itapunguza kasi ya watu kuhamia mijini inayozikabili miji mingi barani Afrika.

Akizungumzia uwekezaji katika nyanja ya uchumi mdogo, Rais alisema uwekezaji huo ndiyo njia pekee ya kuboresha na kuinua uchumi wa watu wa kawaida huku ikitumia vema soko lake la ndani kwa kutumia bidhaa zinazopatika barani humo badala ya kuendelea kutumia fedha nyingi kuagiza bidhaa kutoka nje, hata zile zinazopatikana nchi jirani.

Rais Kikwete alisema ili kupiga hatua kimaendeleo, Afrika kupitia AfDB na wahisani wengine wa ndani na nje lazima iwekeze katika ujenzi na uboreshaji wa miuondombinu ambayo ni nyenzo muhimu kimaendeleo.

Kuhusu sekta ya utali, alisema licha ya Afrika kujaliwa vivutio vingi vya utalii, sekta hiyo bado haichangii kikamilifu uchumi wa bara hilo kutokana na kukabiliwa na changamoto kadhaa ikiwemo miundombinu mibovu, ukosefu wa safari za ndege za kimataifa na bei kubwa ya safari ndege chache za kimataifa zinazofanya safari zake barani Afrika.


Lowassa na ajira
Novemba 15, mwaka jana akiwa katika harambee ya ujenzi wa Kanisa Katoliki la Mtakatifu Joseph Makasa, Parokia ya Nyakato, Mwanza, Lowassa alionya kuhusu tatizo hilo na kulitaka Kanisa lisaidie kujenga vyuo vya ufundi.

Alitoa takwimu akisema utafiti wa mwaka 2006, ambao hata hivyo, hakusema ulifanywa na taasisi gani, ulionyesha kuwa tatizo hilo kwa sasa limekuwa na kufikia asilimia 15 huku likigusa zaidi vijana wenye umri wa miaka kati ya 15 hadi 24 ambao ndiyo nguvukazi ya taifa.

Novemba 29, mwaka huo wa jana akiwa harambee ya ujenzi wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri (KKKT), Usharika wa Amani Sabasaba, Singida, Lowassa alionya tena kuhusu tatizo hilo la ajira.

Mwezi Machi mwaka huu akiwa katika sherehe za uzinduzi wa Jimbo jipya la Kanisa Katoliki Ifakara alirejea kisema: “Nawaomba maaskofu katika miradi yenu mlipe kipaumbele suala la tatizo la ajira kwa vijana.... hili kama tulivyosema ni bomu linalosubiri kulipuka...”

Hata hivyo, kauli hiyo mpya ya Lowassa, ilijibiwa na Waziri wa Kazi, Ajira na Maendeleo ya Vijana Gaudensia Kabaka Machi 21 akisema, "Siyo kweli kudai Serikali hayaijafanya kitu, wanakuwa hawaitendei haki na kuongeza kwamba, utafiti uliofanywa na wizara yake kwa kushirikiana na Taasisi ya Takwimu ya Taifa (NBS), unaonyesha kuwa tatizo hilo limepungua kwa asilimia 1.2.

No comments:

Post a Comment